• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Kanisa lakosoa chanjo ya lazima

Kanisa lakosoa chanjo ya lazima

Na MERCY MWENDE

KANISA Katoliki limepinga pendekezo la serikali kuwa raia wote wanaotafuta huduma za umma wapate chanjo dhidi ya Covid-19 kwa lazima.

Akizungumza mjini Nyeri wakati wa sherehe za Krismasi mnamo Jumamosi, Askofu wa Dayosisi ya Katoliki Jimbo la Nyeri Bw Anthony Muheria, alisema ingawa hatua hiyo bado haijatekelezwa, inaenda kinyume na haki za binadamu.

Askofu Muheria alieleza kuwa uamuzi huo ulifikiwa kufuatia mkutano wa maaskofu wa kanisa Katoliki nchini.

“Kwa sasa ni asilimia tisa tu ya wananchi ambao wamechanjwa. Ina maana kuwa asilimia kubwa ambayo bado haijapokea chanjo itanyimwa huduma za umma,” akasema.

Licha ya maambukizi ya virusi vya Covid-19 kuendelea kuenea nchini, Askofu Muheria aliwalaumu wanasiasa kwa kuendeleza mikutano yao ya kampeni za kisiasa, jambo ambalo lliliwaweka raia hatarini zaidi.

Alieleza ilikuwa si haki kwamba baadhi ya wananchi waliohudhuria mikutano hiyo walikosa uwezo wa kugharamia malipo ya hospitali endapo wangeugua.

Katika hotuba yake, Askofu Muheria alibaini kuwa Kanisa Katoliki halikupingana na chanjo ya Covid-19 ila kulikuwa na njia bora za kuwahamasisha raia waipokee chanjo.

Aliitaka serikali ishirikiane na washirikishi wa kidini na mashirika yasiyo ya serikali (NGOs) katika kuzitafuta njia bora za kuwafanya wakenya wapate chanjo.

You can share this post!

Jorginho afunga penalti mbili na kusaidia Chelsea kuzamisha...

Harry Kane aongoza Spurs kupepeta Crystal Palace katika...

T L