• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
Chepkoech kubeba matumaini ya Kenya kwenye mbio za ukumbini za mita 3,000 nchini Ujerumani

Chepkoech kubeba matumaini ya Kenya kwenye mbio za ukumbini za mita 3,000 nchini Ujerumani

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA wa dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na vidimbwi vya maji, Beatrice Chepkoech anapigiwa upatu wa kutamalaki leo makala ya kwanza ya mwaka huu ya mbio za dunia za ukumbini (World Indoor Athletics Tour) mjini Karlsruhe, Ujerumani.

Itakuwa mara ya kwanza kwa Chepkoech, aliyetawala mashindano kadhaa katika mwaka wa 2020, kunogesha mbio za msimu huu katika fani ya mita 3,000.

Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 29 amewahi kushiriki mashindano mawili ya awali mjini Karlsruhe ila katika fani yam bio za mita 1,500. Aliambulia nafasi ya tatu mnamo 2018 kabla ya kuridhika na nafasi ya nne mnamo 2020.

Chepkoech ndiye mshikilizi wa rekodi ya kitaifa katika mbio za ukumbini mwa mita 1,500 (dakika 4:02.09) na aliweka muda bora wa binafsi wa dakika 8:22.92 katika mbio za mita 3,000 mnamo 2020.

Kati ya wanariadha wengine wanaotazamiwa kutoana jasho na Chepkoech na kumpa ushindani mkali ni Mkenya Gloria Kite na mtimkaji Fantu Worku wa Ethiopia.

Kite anajivunia muda bora wa dakika 8:29.91 katika mbio za mita 3,000 huku Worku akitarajiwa kutamba baada ya kukamilisha mashindano mawili ya awali kimataifa ndani ya mduara wa sita-bora.

Mbio hizo zimevutia pia wanariadha Melissa Courtney-Bryant, Mirusa Mismas na Elena Burkard kutoa Ujerumani.

Kwa upande wa mbio za mita 200, bingwa wa dunia Asher-Smith atakuwa ulingoni kuendeleza ubabe wake katika fani hiyo ya mbio fupi.

Asher-Smith ambaye hajawahi kushiriki mbio zozote za ukumbini kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, amewahi kutifua kivumbi cha mashindano mengine mjini Karlsruhe mara tatu na akaibuka mshindi mnamo 2015, nafasi ya pili mnamo 2016 na nafasi ya pili mnamo 2017.

Mnamo 2015, Asher-Smith alisajili muda wa sekunde 7:08 na kuambulia nafasi ya pili kwenye mbio za ukumbini za bara Ulaya (European Indoor Championships) jijini Prague, Jamhuri ya Czech. Alisajili muda uo huo mnamo 2018 jijini Glasgow, Scotland. Washindani wakuu wa Asher-Smith watakuwa Ajla del Ponte (Uswisi), Carolle Zahi na Asha Philip aliyetawazwa bingwa wa bara Ulaya mnamo 2017.

Philip, ambaye ni mshikilizi wa rekodi ya kitaifa nchini Uingereza, anajivunia muda bora wa sekunde 7.06. Del Ponte atatarajiwa kuboresha muda wake bora wa sekunde 7.17 baada ya kujivunia msimu wa kuridhisha mnamo 2020. Muda bora na wa kasi zaidi unaojivuniwa na Zahi ni wa sekunde 7.19 aliouweka miaka mitatu iliyopita.

You can share this post!

Serikali sasa yapanga kurudisha kiboko shuleni

Wakazi Lamu wapendekeza barabara na vichochoro kupewa...