• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 3:09 PM
Serikali sasa yapanga kurudisha kiboko shuleni

Serikali sasa yapanga kurudisha kiboko shuleni

GEORGE ODIWUOR na WYCLIFFE NYABERI

MATUMIZI ya kiboko kuwaadhibu wanafunzi watundu yatarudishwa iwapo pendekezo la Wizara ya Elimu litakubaliwa.

Waziri Elimu Profesa George Magoha alidokeza kuwa serikali inatathmini sheria ili kuwaruhusu walimu kuwaadhibu wanafunzi kwa kuwachapa kiboko.

“Tumeanza kutathmini upya adhabu ya viboko baada ya wanafunzi kuonyesha tabia mbaya, na huenda hivi karibuni tukawaruhusu walimu kutumia kiboko. Pengine hili litakomesha ukosefu wa nidhamu,” akasema Prof Magoha akiwa katika Kaunti ya Kisii, Alhamisi.

Alisema iwapo hilo litakubaliwa, walimu watatakikana kutumia kiboko kwa njia ya kadri ili kuepuka kuwaumiza wanafunzi.

Matumizi ya kiboko kuwaadhibu wanafunzi yalipigwa marufuku mnamo 2001 kupitia ilani iliyotolewa na aliyekuwa waziri wa elimu wakati huo Kalonzo Musyoka baada ya kupitishwa kwa sheria ya watoto kwa msingi kuwa kiboko ni ukiukaji wa haki za binadamu.

Katika juhudi zaidi za kukabiliana na utovu wa nidhamu shuleni, Prof Magoha alifichua kuwa serikali itazindua oparesheni ya kuwapima wanafunzi kote nchini kutambua wanaotumia dawa za kulevya.

“Maafisa wa Wizara ya Afya wataanza kutembelea shule mbalimbali kukusanya sampuli za damu kutoka kwa wanafunzi zipimwe kubaini ikiwa zina chembechembe za dawa za kulevya. Ikiwa chembechembe za dawa za kulevya zitapatikana kwenye damu, mwanafunzi husika atalazimika kueleza alivyozipata,” akaeleza waziri.

Kulingana na Prof Magoha, wanafunzi walitumia kipindi walichokuwa nyumbani kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya kama vile bangi na pombe.

Aliongeza kuwa huenda dawa pia zinaingizwa shuleni kisiri na ndizo huchochea wanafunzi kuchoma shule na kushirikisha vitendo vingine vya utovu wa nidhamu.

Kiboko. Picha/ AFP

Prof Magoha pia alisema wizara yake inafanya mazungumzo na Idara ya Kupeleleza Uhalifu (DCI) kwa lengo la kuwatambua wanafunzi ambao hushiriki visa vya uhalifu.

“Huu mwenendo wa kihayawani unatoka wapi? Mkumbuke kuna Huduma Namba, kwa hivyo kuwapata itakuwa rahisi sana,” Waziri akaonya.

Aliwaonya wanafunzi kuwa hawawezi kutumia umri wao mdogo kama kisingizio cha kufanya vitendo vya uhalifu.

You can share this post!

Fundi mjengo afichua siri kali ya buda

Chepkoech kubeba matumaini ya Kenya kwenye mbio za ukumbini...