• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 PM
Chipukizi William Saliba kuwa kizibo cha beki David Luiz kambini mwa Arsenal

Chipukizi William Saliba kuwa kizibo cha beki David Luiz kambini mwa Arsenal

Na MASHIRIKA

KOCHA Mikel Arteta wa Arsenal amesema kwamba kuondoka kwa beki mzoefu David Luiz, 34, ugani Emirates mwishoni mwa msimu huu kutampa fursa maridhawa ya kuisuka upya safu ya ulinzi ya kikosi hicho huku nafasi ya Luiz ikitarajiwa kujazwa na chipukizi raia wa Ufaransa, William Saliba.

Ingawa Arsenal walimsajili Saliba, 20, kwa Sh3.8 bilioni mnamo 2019 kutoka Saint-Etienne ya Ufaransa, sogora huyo hajawahi kuwachezea katika mchuano wowote akivalia jezi za kikosi cha kwanza.

Alisalia kambini mwa St-Etienne kwa mkopo mnamo 2019-20 na akarejea Emirates alikotegemewa zaidi katika kikosi cha chipukizi wa U-23 kabla ya kutumwa kambini mwa Nice kwa msimu mwingine mmoja wa mkopo.

Licha ya kukabiliwa na majeraha ya mara kwa mara muhula huo, Saliba alichezea St-Etienne mara 17 katika mapambano yote na akaongoza kikosi hicho kutinga fainali ya French Cup dhidi ya PSG.

Ingawa Luiz hajafichua mipango yake ya baadaye, sogora huyo wa zamani wa Chelsea na Paris Saint-Germain (PSG) anapigiwa upatu kusalia nchini Uingereza kuendelea kusakata soka ya Ligi Kuu ya EPL.

Hata hivyo, maarifa yake tayari yameanza kuhemewa na Benfica ya Ureno, Lazio ya Italia na vikosi kadhaa vya Major League Soccer (MLS) nchini Amerika.

Luiz aliingia katika sajili rasmi ya Arsenal mnamo Agosti 2019 baada ya kuagana na Chelsea kwa kima cha Sh1.1 bilioni. Amekosa kuwa sehemu ya kikosi ambacho kimetegemewa na Arsenal katika jumla ya michuano minne iliyopita kutokana na jeraha la paja.

Chini ya Arteta ambaye ni raia wa Uhispania, Arsenal kwa sasa wanashikilia nafasi ya tisa kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 55, tisa nyuma ya Chelsea wanaofunga orodha ya nne-bora.

Luiz alijitosa katika ulingo wa soka ya kitaaluma mnamo 2001 ambapo alichezea klabu ya Vitoria nchini Brazil kabla ya kusajiliwa na Benfica ya Ureno iliyojivunia huduma zake kuanzia mwaka wa 2007 hadi 2010.

Sogora huyo aliingia katika sajili rasmi ya Chelsea mnamo Januari 2011 na akaongoza kikosi hicho kutwaa taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2011-12 na Europa League msimu uliofuata.

Alisajiliwa na Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa kwa Sh7 bilioni mnamo Juni 2014 na akaweka rekodi ya kuwa beki ghali zaidi duniani wakati huo. Alinyanyua mataji manne ya soka ya Ufaransa katika kipindi cha misimu miwili aliyochezea PSG na akarejea Chelsea mnamo Agosti 2016 kwa kima cha Sh4.2 bilioni kabla ya kutua ugani Emirates.

Luiz alishindia Chelsea taji la EPL, ubingwa wa Europa League na makombe mawili ya FA katika awamu yake ya kwanza ugani Stamford Bridge.

Alisaidia Arsenal kutia kapuni ubingwa wa Kombe la FA mnamo 2019-20 ambapo walikomoa Chelsea 2-1 kwenye fainali iliyowakutanisha ugani Wembley, Uingereza. Alikuwa pia sehemu ya kikosi cha Arsenal kilichopepeta Liverpool kupitia penalti mwanzoni mwa msimu huu na kutia kibindoni taji la Community Shield.

Luiz aliwajibishwa na timu ya taifa ya Brazil kwa mara ya kwanza mnamo 2010. Tangu wakati huo, amechezea mabingwa hao mara tano wa dunia mara 50.

Alikuwa sehemu ya kikosi cha Brazil kilichotwaa taji la FIFA Confederations Cup mnamo 2013 na kutinga nusu-fainali za Kombe la Dunia mnamo 2014. Aliwakilisha Brazil kwenye makala mawili yaliyopita ya kipute cha Copa America.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Hatuna ulazima wowote wa kumtimua kocha Pirlo –...

Van Dijk athibitisha kwamba hatachezea Uholanzi kwenye...