• Nairobi
  • Last Updated May 14th, 2024 3:52 PM
Chogo alenga kufikia kiwango cha nyota Cristiano Ronaldo wa Manchester United

Chogo alenga kufikia kiwango cha nyota Cristiano Ronaldo wa Manchester United

Na PATRICK KILAVUKA

KIJANA Gideon Chogo, 23, ni winga wa kulia wa UoN Olympic ambaye amejifunga kibwebwe kuhakikisha anahimili dhoruba za kusakata boli ili kujikuza si tu katika michezo lakini pia afikie malengo yake ya kiafya na kimasomo.

Anasema anatambua boli kuwa njia ya kusawazisha mambo kwa maisha yake kwani kwa kufanya mazoezi, kunamwezesha kuwa fiti kiafya, ari ya kucheza imempa fursa kutangamana na wachezaji na mashabiki wa kutoka jamii tofauti na kujifunza mengi kuhusu mitindo ya maisha yao mbali na kusawazisha mawazo baada ya kufanya mtihani au iwapo anajihisi kutomakinika vizuri.

Mwanadimba huyu ni mwanafunzi wa Fizikia na Hisabati Chuo Kikuu cha Nairobi.

Mwanasoka Gideon Chogo wakati wa mechi dhidi ya FC Talents katika uwanja wa Kihumbuini. PICHA | PATRICK KILAVUKA

Alisomea Shule ya Msingi ya Agbon Academy, Nairobi kabla kusajiliwa na Sekondari ya Rongena, Kaunti ya Narok.

Alianza kusakata mpira kuanzia shule ya msingi na kufika kiwango cha Kaunti ya Nairobi kabla kuendeleza weledi wake wa soka akiwa shule ya upili ambapo alishiriki michezo ya shule za upili, Kilgoris, Kaunti ya Narok.

Kuchochea talanta yake zaidi, alishiriki timu ya Ruai United, Rongena FC kisha UoN Olympic.

Alihusishwa kikamilifu katika Ligi ya Kaunti ya FKF, Nairobi West na aliweza kucheka na nyavu mara sita msimu uliopita na wakati wa kuandika makala haya alikuwa ametia kimia mabao matatu.

Kocha ambaye anamsifu kwa kumtoka maruerue ya soka ni Isaac Mwendo ambaye pia alikuwa mwalimu wake akiwa shule ya upili akichezea timu ya Kisukioni, Tala, Kaunti ya Machakos.

Mwanasoka ambaye huwa hampi usingizi kucheza mithili yake ni Cristiano Ronaldo wa Manchester United kutokana na mfumo wake wa uchezaji, pasi za uhakika, mipira mirefu anayoipiga na ustadi wake wa kupachika magoli.

Angependa kupeperusha bendera katika timu ya AFC Laeopards au Wazito FC hapa nchini kabla kuzamia kuvalia jezi la Manchester United.

Sapoti ya kujikuza kwake kisoka kunatokana na mzazi na babuye ambao wanahakikisha hakosi buti, jezi na nauli jambo ambalo linamtia moyo wa kupata ushindi siku zijazo.

Angependa timu yake ijitanue zaidi angalau aicheze katika ligi za hadhi kabla yeye kusaka majani mabichi ughaibuni.

Rai yake ni kwa wasimamizi wa Shirikisho la Kandanda Nchini ni kwamba, watupe jicho mashinani kuvua vipawa bila kukariri kwamba hamna talanta nchini ilhali kuna vipaji kochokocho. Pia, wakuze akademia za kandanda kila kaunti ndogo.

Kwa wachezaji ni kwamba wasikate tamaa, wasipoteza tumaini japo changamoto zipo na wawe na mtazamo mzuri katika fani ya soka.

 

  • Tags

You can share this post!

Kalonzo abaki mpweke Raila, magavana wakisusia mkutano

EPL: Everton walaza Leicester na kujiondoa katika hatari ya...

T L