• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Colombia na Venezuela waambulia sare tasa kwenye Copa America

Colombia na Venezuela waambulia sare tasa kwenye Copa America

Na MASHIRIKA

COLOMBIA walisalia katika nafasi ya pili katika Kundi B kwenye mashindano ya Copa America baada ya kuambulia sare tasa dhidi ya Venezuela katika mchuano wao wa pili nchini Brazil usiku wa Ijumaa.

Colombia walishuka dimbani wakitarajiwa kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 1-0 dhidi ya Ecuador katika mchuano wao wa kwanza wa Kundi B mjini Cuiaba, Brazil mnamo Juni 15.

Ingawa hivyo, mpango wao ulivurugwa na Venezuela waliojibwaga uwanjani wakipania pia kuepuka kichapo cha pili mfululizo kwenye Copa America baada ya Brazil kuwanyeshea kwa magoli 3-0 katika mchuano wa ufunguzi wa Kundi B.

Colombia walianza mechi kwa matao ya juu huku wakitamalaki mechi na kumiliki asilimia kubwa ya mpira. Walisuka na kukamilisha idadi kubwa zaidi ya pasi (563) ikilinganishwa na Venezuela waliokamilisha pasi 301 pekee.

Hata hivyo, mchuano huo ulitawaliwa na hisia kali huku jumla ya kadi tano za manjano zilitolewa kwa wanasoka wa Venezuela na Colombia kuonyeshwa kadi hizo mara mbili. Mambo yaliwaendea Colombia visivyo mwishoni mwa kipindi cha pili baada ya mwanasoka Luis Diaz kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 90.

Colombia kwa sasa wanajivunia alama nne kwenye msimamo wa Kundi B huku pengo la pointi mbili likitamalaki kati yao na viongozi Brazil. Venezuela wanakamata nafasi ya tatu kwa alama moja mbele ya Ecuador na Peru ambao hawana pointi yoyote.

Colombia watamenyana na Peru katika mchuano wao ujao mnamo Juni 21 kabla ya kufunga kampeni za Kundi B dhidi ya Brazil ambao ni mabingwa watetezi mnamo Juni 24, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

  • Tags

You can share this post!

Man-City yatoa ofa ya mwisho ya Sh15.6 bilioni kushawishi...

UHURU AFYEKEA RAILA NJIA