• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Man-City yatoa ofa ya mwisho ya Sh15.6 bilioni kushawishi Harry Kane kutoka Spurs

Man-City yatoa ofa ya mwisho ya Sh15.6 bilioni kushawishi Harry Kane kutoka Spurs

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City wamewasilisha ofa ya mwisho ya Sh15.6 bilioni kumshawishi fowadi na nahodha Harry Kane kuagana na Tottenham Hotspur.

Kwa mujibu wa gazeti la Mirror Sport, Man-City ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) watajiondoa katika vita vya kufukuzia maarifa ya Kane iwapo Spurs watakataa kumwachilia Kane kutua ugani Etihad kwa kiasi hicho cha fedha.

Kulingana na taarifa waliyoitoa mnamo Juni 19, 2021, Man-City hawako radhi kusubiri hadi siku ya mwisho kumsajili Kane, 27. Matarajio yao ni kukamilisha mapema mchakato wa kusajili wachezaji wapya ili wawe sehemu ya maandalizi yao kabambe kwa ajili ya msimu mpya wa 2021-22.

Kinachosubiriwa sasa ni kuona iwapo Spurs ya mwenyekiti Daniel Levy itakubali ofa hiyo ya Man-City au la. Awali, Levy alisisitiza kwamba kikosi chochote kinachomezea mate huduma za Kane kingelazimika kuweka mezani kima cha Sh23 bilioni. Aidha, alishikilia kuwa Spurs wasingekuwa radhi kushuhudia Kane akijiunga na washindani wao wakuu kwenye EPL.

Mwanzoni mwa Mei 2021, Kane aliwafichulia Spurs kuhusu nia yake ya kuagana nao rasmi ili ajiunge na kikosi kitakachompa jukwaa maridhawa la kuanza kushinda mataji.

Tangazo hilo lilichochea vikosi vya Man-City, Manchester United, Chelsea, Real Madrid na Barcelona kuanza kuyahemea maarifa ya supastaa huyo raia wa Uingereza ambaye kwa sasa anawaniwa pia na Paris Saint-Germain (PSG) wanaotiwa makali na kocha Mauricio Pochettino aliyewahi kumnoa Kane kambini mwa Spurs.

Akihojiwa na Sky Sports, Kane alifichua kwamba azma yake ni kusalia katika soka ya EPL japo alitaka masuala yote yanayofungamana na mustakabali wake kitaaluma kushughulikiwa na Spurs kabla ya kipute cha Euro kukamilika mnamo Julai 11.

Mbali na Kane, Man-City wanawania pia maarifa ya wanasoka Erling Braut Haaland wa Borussia Dortmund na Danny Ings wa Southampton. Kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola kinamsaka fowadi atakayekuwa kizibo cha Sergio Aguero ambaye tayari amesajiliwa na Barcelona ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Sonia: Chipukizi anayelenga nyayo za Priyank Chopra

Colombia na Venezuela waambulia sare tasa kwenye Copa...