• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
DIMBA MASHINANI: Kigogo mchezo wa jadi usiobagua umri, hadhi

DIMBA MASHINANI: Kigogo mchezo wa jadi usiobagua umri, hadhi

Na CHARLES ONGADI

MCHEZO wa bao ama kigogo ni wa tangu jadi jimbo la Pwani na unazidi kupendwa na watu wa matabaka yote hasa wazee.

Ni mchezo unaoashiria utamaduni wa Mpwani na unachezwa mara baada ya kazi ya siku kutwa hasa nyakati za jioni.

Aghalabu utawapata wazee kwa vijana wakicheza mchezo huu katika ‘maskani’ za kunywa kahawa wakishindana na wakati huo huo kubadilishana mawazo ya kimaendeleo.

Ni mchezo unaochezwa na watu wawili kwenye gogo lililochongwa kiumaridadi na lililo na mashimo 14 yaliyogawanywa sehemu mbili, kila upande kukiwa na mashimo saba.

Kati ya mashimo haya saba, manne kati yayo hutiwa mburuga nne katika kila shimo na kubakisha mashimo matatu na hapo ndipo mchezo huanza kwa kuzungusha mburuga katika kila shimo.

Hapa kinyang’anyiro huwa ni kung’ang’ania kode tano (bibi) ambapo anayeibuka na mburuga nyingi katika kila mchuano ndiye mshindi na hupewa ‘bibi’ mmoja.

Mshindi wa ‘bibi’ wote watano ndiye hutawazwa mshindi na huhitajika kuchuana na mwingine kumsaka bingwa halisi wa siku.

Klabu ya Majaoni Mugogo Kigogo inayopatikana eneo la Majaoni, Bamburi katika kaunti ndogo ya Kisauni, ni kati ya klabu kongwe zaidi katika jimbo la Pwani katika mchezo huu.

Ina zaidi ya wanachama 50 walio na umri kati ya miaka 18-76 wanaokutana kila jioni kuchuana katika kujiweka sawa kabla ya kushiriki mashindano.

“Klabu hii ilianzishwa mwaka wa 1978 na Emmanuel Karisa Maitha (marehemu) kwa nia ya kudumisha michezo yetu ya kale kwa vizazi vijavyo”, asema Kitsao Salehe Kabuni almaarufu Bokassa.

Kwa mujibu wa Bokassa, Emmanuel Karisa Maitha ambaye baadaye aliibuka kuwa diwani wa Bamburi kisha mbunge wa Kisauni kabla ya kuhudumu kama Waziri wa Utalii na Wanyama wa Porini, alikuwa mpenzi mkubwa wa mchezo huu.

“Umaarufu wa Maitha ulianzia hapa na hata alipokuwa Waziri, alikuwa na mazoea ya kuja hapa kila wikendi kucheza mchezo huu”, afichua Bokassa wakati wa mahojiano na Dimba.

Aidha, Mumba Gandi almaarufu Mzee Kingi Kitsao ambaye ni mmoja kati ya wachezaji wakongwe wa Kigogo jimbo la Pwani, anasema huu ni mchezo unaodokeza utamaduni wa jamii ya Wamijikenda.

Mzee Mumba pamoja na Jeremia Katana Gona na James Maitha (marehemu) walitambuliwa sana miaka ya awali kutokana na uhodari wao katika mchezo huu.

Kalume Baya, 23, anasema alivutiwa na mchezo huu tangu akiwa na miaka 12 alipokuwa akiandamana na babaye ambaye ni shabiki na mchezaji kuangalia mchezo huu eneo la Miritini.

Kalume; “Huu si mchezo wa wazee kama wengine wanavyodhani bali hata sisi vijana tunaupenda.”

Klabu ya Majaoni Mugogo Kigogo imeshiriki mashindano mengi tangu kuanzishwa kwake ikizuru miji tofauti Pwani kama Malindi, Kilifi na Kwale kwa michuano mbalimbali.

Mwaka juzi, klabu hii ilichuana na wenzao kutoka Malindi katika mechi iliyovutia halaiki kubwa ya mashabiki wa mchezo huu.

Bokassa asema kwa kipindi kirefu klabu ya Majaoni Mugogo Kigogo imetawala mchezo huu jimbo la Pwani kutokana na kuwepo kwa wachezaji wakongwe na wenye uzoefu.

You can share this post!

Karua apendekeza wakati wa uchaguzi kuwe na maafisa maalum

Fainali za Copa America sasa zakosa mwenyeji baada ya...