• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
DIMBA MASHINANI: Kipendacho roho ni dawa; kwa Aura voliboli dozi tosha

DIMBA MASHINANI: Kipendacho roho ni dawa; kwa Aura voliboli dozi tosha

Na CHARLES ONGADI

VOLIBOLI ya walemavu, Sitting Volleyball, imeibukia kuwa kimbilio la walemavu wengi wenye ari ya kudhihirisha uwezo wao michezoni.

Inatofautiana na voliboli ya kawaida kutokana kwamba inachezwa wachezaji wakiwa wameketi chini kwenye zulia maalum.

Wanatumia neti yenye urefu wa mita 9.7, upana wa mita 0.8 na kimo cha mita 1.15 kwa wanaume au mita 1.05 kwa akina dada. Uwanja wenyewe huwa urefu mita 10 na upana mita 6. Mojawapo ya sheria muhimu ni kwamba sehemu ya makalio ya mchezaji ni lazima iwe chini sakafuni anapocheza.

Mchezo huu ulianzishwa mnamo 1956 nchini Uholanzi kwa minajili ya wanajeshi waliojeruhiwa vitani. Muda si muda mnamo 1958 mashindano ya kwanza ya kimataifa yaliandaliwa baina ya klabu za kutoka Ujerumani na Uholanzi.

Aidha, mchezo huu ulishirikishwa kwa mara ya kwanza katika Olimpiki, Paralympics, kwa upande wa wanaume mnamo 1980; kabla ya kinadada kujumuishwa baadaye 2004 .

Nchini Kenya, Jackline Akinyi Aura, 35, ni kati ya wachezaji hodari wa kike wa voliboli ya walemavu anayevuma kama papa baharini. Kiu ya kucheza voliboli ilimuanza akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi ya Sianda mjini Kisumu, ila hakucheza sababu ya ulemavu.

“Nilitamani kucheza lakini walimu na wanafunzi waliamini singeweza kutokana na hali yangu,” asema Akinyi, aliyepata ulemavu akiwa mtoto miaka minne baada ya kuugua polio na kupooza mguu wa kulia.

Licha ya kubaguliwa shuleni alizidi kujiamini na kukataa kuponza ari yake ya michezo. Mapenzi yake kwa voliboli yalimfanya kuhudhuria kila shindano, na kuwa miongoni mwa mashabiki sugu wa timu ya shule.

Hatimaye ndoto ya Akinyi ilitimia 2009 mara baada ya kukamilisha masomo ya upili na kutua jijini Nairobi kutafuta ajira.

“Sikujua kuna voliboli mahsusi kwa walemavu hadi nilipopata mwaliko kutoka kwa kocha wa timu ya taifa, tulipokutana ndani ya matatu na kuniomba kuhudhuria mazoezi ya uwanjani Kasarani,” asimulia mama huyu wa watoto wanne.

Kwa ari iliyomjaa, mazoezi ya wiki tatu yalitosha kuelewa kanuni za mchezo.

“Sikutatizwa kwa sababu kipendacho roho ni dawa, na voliboli ni mchezo niliopenda tangu utotoni.”

Alijikuta katika timu ya taifa iliyoshiriki mashindano ya voliboli ya walemavu Afrika Mashariki nchini Rwanda mwaka 2009. Akiwa na wenzake kama Jane Adhiambo, Doris Atieno, Linet Achieng’, Rael Mara na Mary Atieno waliunda kikosi imara kilichotifua kivumbi katika mashindano hayo yaliyojumuisha nchi za Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Lakini ndoto yake kuwakilisha taifa mwaka 2010 nchini Uholanzi ilizima Kenya ilipojiondoa kwa ukosefu wa hela. Akaamua kuyoyomea Mombasa mnamo 2013 baada ya kupata mwaliko wa timu ya kaunti iliyokuwa ikifanya mazoezi katika ukumbi wa Aga Khan chini ya kocha Anthony Odhiambo.

Alifaulu kuongoza kikosi hicho kunyanyua ubingwa wa mashindano ya kaunti mjini Meru mwaka 2013.

“Timu yetu ilifanya vizuri kutokana na sapoti nzuri ya Gavana Hassan Joho iliyoleta motisha kikosini,” aeleza Akinyi.

Akinyi anakiri kwamba wanavoliboli walemavu wamekuwa wakipitia changamoto nyingi hasa ukosefu wa vifaa maalum vya mazoezi, ukumbi wa kisasa, miundomsingi ya usafiri na kutolipwa marupurupu licha ya kupeperusha vyema bendera ya Kenya kimataifa.

 

You can share this post!

Usalama waimarishwa katika mpaka wa Kenya na Somalia...

MBWEMBWE: Kante: Shabiki sugu wa tenisi, anachotewa mihela...