• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
MBWEMBWE: Kante: Shabiki sugu wa tenisi, anachotewa mihela ya kutisha

MBWEMBWE: Kante: Shabiki sugu wa tenisi, anachotewa mihela ya kutisha

Na CHRIS ADUNGO

N’GOLO Kante, 29, ni kiungo raia wa Ufaransa anayechezea Chelsea katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Baada ya kuridhisha kambini mwa Boulogne mnamo 2012, Kante alisajiliwa na Caen bila ada yoyote mnamo 2013 na kusaidia kikosi hicho kufuzu kwa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).

Aliwahudumia Caen hadi 2015 aliposajiliwa na Leicester City kwa kima cha Sh784 milioni mnamo 2015. Ushawishi wake uwanjani King Power ulisaidia Leicester kunyanyua taji la EPL msimu wa 2015-16; naye akatawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka akiwa hapo chini ya kocha Claudio Ranieri.

Mnamo 2016 Kante aliingia katika sajili rasmi ya Chelsea kwa kima cha Sh4.5 bilioni. Aliongoza Blues kutia kibindoni ufalme wa EPL mnamo 2016-17 akiibukia kuwa kiungo wa kwanza mkabaji, baada ya Eric Cantona mnamo 1992 na 1993, kutwaa taji la EPL misimu miwili mfululizo akivalia jezi za klabu tofauti.

Kante aliwajibishwa na timu ya taifa ya Ufaransa kwa mara ya kwanza mnamo 2016 wakiambulia nambari mbili nyuma ya Ureno katika dimba la Euro 2016.

Mnamo 2017 kiungo huyo alitawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka nchini Ufaransa, hiyo ikiwa mara ya kwanza baada ya miaka saba kwa sogora wa EPL kutia kibindoni taji hilo.

Miezi 12 baadaye, alisaidia timu yake ya taifa kupepeta Croatia 4-2 na kunyanyua Kombe la Dunia nchini Urusi.

Kante aliambulia nafasi ya nane kwenye tuzo ya Ballon d’Or mnamo 2017 kabla kuorodheshwa wa 11 kwenye kinyang’anyiro hicho cha kuwania taji la Mwanasoka Bora Duniani mwaka 2018.

Utajiri

Baada ya Ben Chilwell, Kai Havertz na Timo Werner, Kante ni miongoni mwa wanasoka wanaokamilisha kundi la pili la wenye ujira mkubwa zaidi ugani Stamford Bridge.

Hususan, Kante kwa sasa anatia kibindoni Sh24 milioni kwa wiki; malipo yanayowiana na yale ya kipa ghali zaidi duniani, Kepa Arrizabalaga.

Thamani ya mali ya Kante inakadiriwa kufikia kima cha Sh4.7 bilioni. Hadi alipojiunga na Chelsea, aliorefusha mkataba wake kwa miaka mitano mnamo Novemba 2018, Mfaransa huyo alikuwa akila Sh18 milioni kila wiki pale Leicester.

Vile vile, hupokea pia donge la hadi Sh360 milioni kwa mwaka kwa kuwa balozi wa bidhaa na huduma za Nike, inayounda vifaa vya michezo mbalimbali.

Isitoshe, Kante pia ni balozi wa kampuni ya vipodozi ya Cover Girl Cosmetics ambayo humpokeza zaidi ya Sh12 milioni kwa mwezi. Mchumba wake, Jude Littler, 46, anamiliki misururu ya mikahawa jijini Paris, Ufaransa.

Kante hujirinia fedha nyinginezo za marupurupu na bonasi ya kusajili sare au kushinda mechi za klabu na timu ya taifa.

Magari

Kwa mchezaji wa kiwango na haiba yake, kigogo huyu huvutiwa pakubwa na magari ya kisasa yenye kasi ya kupindukia. Baadhi ni Mercedes Benz, Mini Cooper S, Aston Martin, Ferrari, Porshe na Lamboghini ambazo kwa pamoja alifoka Sh118 milioni.

Majengo

Sawa na wachezaji wengine wa kufu yake, Kante anamiliki majumba mengi ya kifahari. Moja ni kasri la Sh620 milioni jijini London, Uingereza, anakoishi na mkewe. Pia ana jengo la Sh550 milioni analotumia kwa biashara jijini Paris.

Familia

Kante alizaliwa Machi 29, 1991, viungani mwa jiji la Paris, Ufaransa. Wazazi wake walihamia Ufaransa kutoka Mali mnamo 1980. Msomi huyu wa uhasibu ni shabiki sugu wa mchezo wa tenisi.

Alianza kutoka kimapenzi na Littler mnamo Machi 2020, miaka sita baada ya mama huyo wa watoto watatu kutalikiana na mwanasoka wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa, Djibril Cisse, 39.

Kipusa huyo kwa sasa ni mjamzito.

Alilelewa na kukulia katika eneo la Rueil-Malmaison, Huats-de-Seine, Ufaransa. Wazazi wake walihamia nchini Ufaransa kutoka Mali mnamo 1980.

Babake mzazi aliaga dunia pindi baada ya Kante kutimu umri wa miaka 11, naye kakake mkubwa, Niama, akafariki kutokana na maradhi ya moyo kabla ya fainali za Kombe la Dunia za 2018 nchini Urusi.

Kabla ya kusajiliwa na Boulogne mnamo 2010, Kante ambaye ni msomi wa masuala ya uhasibu na shabiki sugu wa mchezo wa tenisi, alikuwa amevalia jezi za kikosi cha JS Suresnes jijini Paris kuanzia mwaka wa 1999.

Kante alianza kutoka kimapenzi na kipusa Jude Littler mnamo Machi 2020, miaka sita baada ya mama huyo wa watoto watatu kutalikiana na mwanasoka wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa, Djibril Cisse, 39.

Jude ambaye kwa sasa ni mjamzito, anatarajia mtoto wa nne baada ya uhusiano wake wa awali na Cisse anayemchumbia kichuna Marie-Cecile Lenzini kujaliwa watoto Prince Kobe, Cassius Clay na Marley Jackson.

You can share this post!

DIMBA MASHINANI: Kipendacho roho ni dawa; kwa Aura voliboli...

Rais Kenyatta aungana na viongozi wengine Dodoma kumuenzi...