• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
DIMBA NYANJANI: Karate ya ‘chini kwa chini’ ya Kenpo yanasua vijana Pwani

DIMBA NYANJANI: Karate ya ‘chini kwa chini’ ya Kenpo yanasua vijana Pwani

Na CHARLES ONGADI

MCHEZO wa kenpo unazidi kupata umaarufu kila uchao miongoni mwa vijana wa Pwani na taifa kwa ujumla.

Ni mchezo unaofanana na ule wa karate ila unahusisha makabiliano ya chini kwa chini .

Ni mchezo ulioanzishwa nchini na Mwamerik mwenye asili ya weusi, marehemu Grand Amen K Raha alipozuru Pwani zaidi ya miaka kumi iliyopita.

Mkufunzi Paul Osawa ndiye alirithi mikoba ya mwendazake, na anaeleza kuwa mchezo huu umechangia kuzuia vijana wengi kujitosa katika maovu ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya, mimba na ndoa za mapema.

Ali Said mwenye umri wa miaka 24 ni miongoni mwa vijana katika mtaa wa Kongowea, Mombasa, ambao kiduchu ajiunge na magenge yasiyofaa kama si mchezo huo.

“ Kama si kenpo pengine ningekuwa mitaani nikitafuna Mogoka ama kutumia ‘unga’, lakini namshukuru Mwenyezi Mungu kwa hili,” atanguliza Ali, ambaye ndiye nahodha wa klabu ya Kongowea Kenpo inayoshiriki Ligi Kuu ya mchezo huu.

Mara baada ya kukamilisha masomo ya upili 2016, kijana huyo aliamua kujitosa mzimamzima katika kenpo.

“Nilianza mazoezi nikiwa shule ya upili lakini singeshiriki kikamilifu sababu ya shughuli za masomo,” alisema na kuongeza kuwa ameimarika hadi kiwango cha Mkanda wa Hudhurungi (Brown Belt).

Ali alivutiwa na mchezo wa kenpo kutokana kwamba umechanganya staili nyingi za kupigana.

Mazoezi yake pia yanampa mtu ujuzi unaomfaa maishani, hususan ujanja wa kukabiliana na wahuni mitaani.

Anawavulia kofia wazazi wake kwa kumsaidia kwa hali na mali ili kufikia malengo yake katika mchezo huu.

Kulingana na Ali, wazazi wake kamwe hawakosi kuhudhuria mashindano anayoshiriki ili kumshangilia na kumpa moyo kuendelea.;

“Kila ninapowaona wazazi wangu ukumbini wakinishangilia huwa najitahidi kuhakikisha nimeibuka mshindi,” alieleza.

Kwa mujibu wa mkufunzi mkuu wa klabu ya Kongowea, Paul Osawa, kijana Ali ni kati ya wachezaji wake tegemeo anaotarajia kuwapandisha gredi katika hafla itakayoandaliwa mwezi Aprili.

Katika mashindano ya Ligi Kuu mkondo wa mwisho yaliyoandaliwa mjini Ruiru, Ali alionesha makeke yake na kuibuka bingwa kwenye mapigano yake yote.

Alieleza Dimba kwamba hatapumzika hadi atakapofikia malengo yake ya kumiliki Mkanda Mweusi (Black Belt) na kuwakilisha taifa katika mashindano ya kimataifa.

Kati ya changamoto anazokabilana nazo kwa sasa ni kukosa muda mzuri wa kufanya mazoezi sababu ya kubanwa na kazi kwani pia ni mfanyabiashara.

Ali, ambaye angali kapera, ana maono kwamba pindi atakapostaafu, atajitosa katika ukufunzi na kuanzisha klabu yake itakayokata kiu ya wapenda mchapano huo.

Anawashauri vijana wenzake wasipoteze muda wao kupiga soga wakitafuna miraa, badala yake wajitose mazoezini kwa minajili ya afya yao.

“Mazoezi ni muhimu hasa kipindi hiki kigumu ambapo ni rahisi kushawishika kuingia katika maovu,” akariri.

Kocha Osawa asema ujio wa Ali katika klabu yake ulichochea vijana wengi kutoka maeneo ya Kongowea, Kidogobasi, Mshomoroni, Kisumu Ndogo, Khadija na mengineo kujitosa katika mchezo huo.

You can share this post!

UDAKU: Kipa De Gea raha tele kuangusha kimalaika

Pesa za wizi hazina maana, akiri pasta