• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Brazil kuwa mwenyeji wa fainali za Copa America

Brazil kuwa mwenyeji wa fainali za Copa America

Na MASHIRIKA

FAINALI za Copa America sasa zitaandaliwa nchini Brazil baada ya Argentina kupokonywa idhini ya kuandaa kinyang’anyiro hicho wiki mbili kabla ya kuanza rasmi.

Shirikisho la Soka la Amerika Kusini (Conmebol) liliondoa fainali za kivumbi hicho nchini Argentina kwa sababu ya kuongezeka kwa visa vya maambukizi ya virusi vya corona.

“Conmebol inashukuru Shirikisho la Soka la Brazil kukubali kuwa wenyeji wa kipute hiki cha Copa America kati ya Juni 13 na Julai 10. Amerika Kusini sasa iko tayari kung’aa nchini Brazil,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Conmebol bila ya kufichua viwanja vitakavyotumiwa kuandalia mashindano hayo.

Awali, Argentina ilikuwa ishirikiane na Colombia kuandaa fainali za Copa America mwaka huu 2020.

Hata hivyo, Colombia walipokonywa idhini hiyo mnamo Mei 20 baada ya kuongezeka kwa visa vya maandamano yaliyochangiwa na hatua ya serikali kuongeza ushuru unaotozwa kwa bidhaa muhimu.

Mnamo Mei 22, serikali ya Argentina ilipiga marufuku safari zote za kuingia na kutoka nchini humo baada ya visa vipya 35,000 vya maambukizi ya corona kuripotiwa siku hiyo.

Kwa upande wao, maandamano ya kulalamikia jinsi janga la corona linavyoshughulikiwa na serikali ya Brazil chini ya Rais Jair Bolsonaro yalifanyika mnamo Mei 29, 2021.

Brazil ambayo imesajili takriban vifo 460,000 kutokana na corona ndiyo nchi ya pili baada ya Amerika ambayo imeathiriwa zaidi na janga hilo duniani.

Brazil ndio mabingwa watetezi wa Copa America baada ya kutia kapuni taji hilo mnamo 2019.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Hedhi salama bado ni changamoto kwa...

PATA USHAURI WA DKT FLO: Mzio wa chakula huletwa na nini?