• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Familia ya mwanariadha Tirop yapinga kupunguzwa kwa mashtaka ya mshukiwa

Familia ya mwanariadha Tirop yapinga kupunguzwa kwa mashtaka ya mshukiwa

TITUS OMINDE Na PATRICIA KIABI

FAMILIA ya mwanariadha wa kimataifa Agnes Tirop imepinga kujihusisha na majadiliano ya kupunguzwa kwa mashtaka na familia ya Ibrahim Rotich ambaye ni mshukiwa mkuu wa mauaji ya mwanariadha huyo.

Akiikabili kesi hiyo siku ya Alhamisi hakimu Reuben Nyakundi aliitaka pande zote mbili kujadiliana na kuona kama watakuwa na msimamo sawa kabla ya kutolewa kwa mwelekeo zaidi wa kesi hiyo.

“Ninawapa nyinyi watu wa pande hizi mbili nafasi ya mwisho kuhusu jambo hili la mashtaka ili nitoe mwelekeo mwafaka,” akaagiza jaji huyo.

Wakati kesi hii ilifika kortini wakili wa mshukiwa, Simiyu Khatete, aliambia korti kuwa mteja wake angependa kuzungumzia kupunguzwa kwa mashtaka ili iwe mashtaka ya mauaji bila ya kukusudia na familia ya marehemu.

“Tulitarajia kutakuwepo na makubaliano baina yetu na familia ya marehemu lakini tumeshangazwa na wao kupinga ombi letu,” alisema Bw Khatete.

Hii ni baada ya wakili anayewakilisha familia, Richard Waringi, kusema kuwa hawajaona stakabadhi zinazoonyesha ombi la kupunguzwa kwa mashtaka.

“Familia ya mwathiriwa haiko tayari kuendelea na ombi la kupunguzwa kwa mashtaka na ikiwa hili litafanyika bado tutaendelea na kesi ya mashtaka ya mauaji yanayomkabili mshukiwa kwa sababu ya mazingira ambayo marehemu alikutana na kifo chake,” alisema Bw Waringi.

Hakimu aliziamuru pande hizo mbili kufika mbele yake Aprili 18, 2023  iwapo watakuwa wamekubaliana kuhusu mashtaka hayo kabla ya kutoa maelekezo zaidi.

Rotich mwenye umri wa miaka 41 ambaye ni mshukiwa mkuu kwa mauaji ya kikatili ya aliyekuwa mke wake alikana mashtaka hayo mbele ya mahakamu kuu baada ya kufanyiwa ukaguzi wa kiakili katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi iliyoonyesha kuwa alikuwa sawa kuendelea na mashtaka.

Mashtaka juu yake yanaonyesha kuwa alimuua Tirop mnamo Oktoba 2 katika mji wa Iten kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Familia ya Tirop ikiongozwa na babake pamoja na ndugu za Rotich walikuwemo wakati wa kikao hiki.

Mshukiwa ambaye anaendelea kuzuiliwa katika gereza la GK Eldoret alikamatwa kwenye kizuizi cha polisi barabarani kwenye mji wa Chaani kule Changamwe akiwa kwenye harakati ya kutorokea nchi jirani baada ya kumuua mwanariadha huyo wa kimataifa.

Mwanariadha huyo alishiriki katika mbio za Olimpiki za mwaka wa 2020 kule Tokyo kwenye mbio za mita elfu tano ambapo alimaliza wa nne

Alipatikana amefariki ndani ya nyumba yake kwenye mji wa Iten mnamo Oktoba 13.

Ripoti ya upasuaji wa maiti iliyofanywa na wataalamu wawili katika Hospitali  ya Rufaa ya Kaunti kule Iten ilionyesha kuwa marehemu alikuwa na majeraha ya kudungwa shingoni na pia aligongwa na kifaa butu kichwani.

Bi Tirop alizikwa nyumbani kwa wazazi wake kaunti ya Nandi tarehe 23 siku ambayo ingefaa aadhimishe miaka 26 ya kuzaliwa.

  • Tags

You can share this post!

Ugaidi: Amerika yaonya raia wake wawe waangalifu nchini...

Njaa kukita kambi nchini, serikali ikiomba raia kusaidiana

T L