• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Ansu Fati sasa kuchezea Barcelona hadi 2027

Ansu Fati sasa kuchezea Barcelona hadi 2027

Na MASHIRIKA

TINEJA matata wa Barcelona, Ansu Fati, 18, ametia saini mkataba mpya wa miaka sita kambini mwa Barcelona ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Kwa mujibu wa kandarasi hiyo mpya, kikosi chochote kitakachotaka kumsajili fowadi huyo chipukizi kutoka Barcelona, sasa kitakuwa na ulazima wa kuweka mezani zaidi ya Sh131 bilioni.

Fati ambaye ni raia wa Uhispania, ana usuli wake nchini Guinea-Bissau. Kwa sasa anavalia jezi nambari 10 mgongoni iliyokuwa ya Lionel Messi aliyeyoyomea Ufaransa kuchezea Paris Saint-Germain (PSG) muhula huu.

Chipukizi huyo alisaidia Barcelona kupepeta Dynamo Kyiv 1-0 mnamo Jumatano usiku ugani Camp Nou na kuweka hai matumaini finyu ya waajiri wake kuingia hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu.

Fati anatarajiwa sasa kuchezea Barcelona hadi 2027. Anakuwa mchezaji wa pili wa Barcelona baada ya Pedri Lopez kutia saini mkataba mpya chini ya kipindi cha wiki moja iliyopita.

Kufikia sasa, Fati amewajibishwa na timu ya taifa ya Uhispania mara nne na amekuwa mchezaji wa Barcelona tangu alipokuwa na umri wa miaka 10 pekee. Alifungia kikosi hicho bao mnamo Septemba katika mchuano uliokuwa wake wa kwanza ligini tangu jeraha la goti limweke mkekani kwa kipindi cha miezi 10.

Anajivunia kuchezea kikosi cha kwanza cha Barcelona jumla ya mechi 47 na kupachika wavuni mabao 15. Aliweka historia ya kuwa mchezaji wa pili mchanga zaidi baada ya Lionel Messi kuwahi kuchezea Barcelona akiwa na umri wa miaka 16 na siku 298. Ndiye mwanasoka mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kufungia Barcelona bao katika kipute cha La Liga.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Wamiliki wa matatu wachangamkia kuondolewa kwa kafyu

Bayern Munich wasubiri hadi dakika za mwisho kusambaratisha...

T L