• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:50 AM
Fowadi Antonio Michail wa West Ham afichua mpango wa kutema Uingereza na kuanza kuchezea Jamaica

Fowadi Antonio Michail wa West Ham afichua mpango wa kutema Uingereza na kuanza kuchezea Jamaica

Na MASHIRIKA

KOCHA David Moyes wa West Ham United amesema fowadi matata wa kikosi hicho, Michail Antonio, bado ana uwezo wa kukichezea timu ya taifa ya Uingereza baada ya kuibuka kwa tetesi kwamba mwanasoka huyo anapania kuanza kusakatia Jamaica.

Antonio, 30, amewahi kutajwa katika kikosi cha Uingereza mara mbili ila bado hajachezeshwa na kikosi hicho katika mechi yoyote.

“Nilisoma kuhusu habari hizo mitandaoni ila sijapata muda wa kuzungumza na Antonio moja kwa moja ili kuzithibitisha,” akatanguliza Moyes.

“Hata hivyo, bado nihahisi kwamba angali na uwezo wa kuteuliwa kuunga kikosi cha Uingereza. Ila isieleweke kwamba napinga maamuzi yake ya kusakatia Jamaica,” akaongeza kocha huyo wa zamani wa Everton, Sunderland, Real Sociedad na Manchester United.

Antonio ana uwezo wa kuchezea Jamaica kutokana na usuli wa wazazi wake na aliwahi kuwaeleza wanahabari mnamo 2016 kwamba alikataa ofa ya kuchezea timu hiyo ya taifa kwa sababu alikuwa na maazimio makubwa ya kuwakilisha Uingereza kimataifa.

Kufikia sasa, Antonio amefungia West Ham jumla ya mabao sita na kuwezesha kikosi hicho kutinga nafasi ya nne kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL). West Ham wamepangiwa kuvaana na viongozi wa jedwali la EPL, Manchester City uwanjani Etihad mnamo Februari 27, 2021.

Wakati uo huo, Moyes mwenye umri wa miaka 57 ameseama kwamba hana nia ya kuagana na West Ham ili kuyoyomea Scotland kudhibiti mikoba iliyoachwa na kocha Neil Lennon aliyeagana na kikosi cha Celtic mnamo Februari 24, 2021 kutokana na matokeo duni ya waajiri wake ligini.

Mkataba wa sasa kati ya West Ham na Moyes ambaye alianza taaluma yake ya ukocha kambini mwa Celtic, unatazamiwa kukatika rasmi mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Biden, Uhuru washauriana kuhusu ushirikiano

Liverpool hawatajishughulisha sana sokoni mwishoni mwa...