• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 5:50 AM
Funga-kazi EPL vikosi vikipigana ya mwisho

Funga-kazi EPL vikosi vikipigana ya mwisho

Na MASHIRIKA

MIKATALE ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) hatimaye inakatwa rasmi hii leo Jumapili kwa mechi 10 tofauti zitakazosakatwa kwa wakati mmoja (6:30pm) katika viwanja mbalimbali.

Manchester City wanaopania kujizolea mataji matatu muhula huu, likiwemo Kombe la FA na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), walihifadhi ufalme wa EPL msimu huu wiki moja iliyopita.

Hiyo ilikuwa baada ya waliokuwa washindani wao wakuu, Arsenal, kukubali kichapo cha 1-0 kutoka kwa Nottingham Forest ugani City Ground na hivyo kupoteza jumla ya mechi sita, kupiga sare sita na kushinda michuano 25 kati ya 37 iliyopita.

Arsenal wamerejea katika soka ya UEFA muhula ujao baada ya kuwa nje ya kipute hicho cha haiba kubwa tangu 2016-17.

Wanashuka ugani Emirates kupimana ubabe na Wolverhampton Wanderers baada ya kujihakikishia nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la EPL.

Kufikia sasa, wanajivunia alama 81, nane nyuma ya Man-City ambao wametawazwa mabingwa wa EPL mara tano katika kipindi cha misimu sita iliyopita chini ya mkufunzi Pep Guardiola.

Mabingwa mara 20 wa EPL, Manchester United, na Newcastle United pia watanogesha soka ya UEFA msimu ujao baada ya kuambulia nafasi za tatu nne mtawalia.

Liverpool (alama 66) na Brighton (62) wana uhakika wa kumaliza kampeni za ligi msimu huu katika nafasi za tano na sita mtawalia na hivyo kufuzu moja kwa moja kwa soka ya Europa League muhula ujao.

Hiyo inaacha Aston Villa (58), Tottenham Hotspur (57) na Brentford (56) katika vita vikali vya kuwania fursa ya kufuzu kwa kipute cha Europa Conference League ambayo ni ligi ndogo zaidi barani Ulaya muhula ujao.

Man-City watavaana leo na Brentford ugani Gtech Community, siku saba kabla ya kumenyana na Man-United kwenye fainali ya Kombe la FA uwanjani Wembley na wiki mbili kabla ya kutua Istanbul nchini Uturuki kupepetana na Inter Milan kwenye fainali ya UEFA uwanjani Ataturk Olympic.

Iwapo watatia kibindoni makombe matatu muhula huu, basi Man-City watafikia rekodi ya majirani zao Man-United waliowahi kutawazwa wafalme wa EPL, UEFA na Kombe la FA katika msimu mmoja wa 1998-99.

Mabingwa hao mara tisa wa EPL, tayari wamenyanyua jumla ya mataji 10, yakiwemo matano ya EPL tangu mikoba yao ianze kudhibitiwa na Guardiola mnamo 2016. Ilivyo, dalili zote zinaashiria kuwa huu ni muhula wao wa kufikisha makombe 12 katika kipindi cha mihula sita chini ya mkufunzi huyo wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich.

Man-City wameshinda mechi 12 mfululizo na kupoteza alama mbili pekee kutokana na michuano 15 iliyopita na ndicho kikosi cha tano kuwahi kunyanyua taji la EPL mara tatu mfululizo baada ya Huddersfield Town (1924-26), Arsenal (1933-35), Liverpool (1982-84) na Man-United waliofanya hivyo mara mbili chini ya Sir Alex Ferguson (1999-2001 na 2007-09).

Macho ya mashabiki yataelekezwa pia zaidi kwa Leeds United, Leicester City na Everton ambao watakuwa katika vita vya kuepuka shoka la kuwateremsha daraja ligini. Southampton, ambao watakuwa wenyeji wa Liverpool ugani St Mary’s, tayari wameshushwa ngazi baada ya kupoteza mechi 25 kati ya 37 zilizopita na kujiokotea pointi 24 pekee.

Leicester watakuwa wenyeji wa West Ham United uwanjani King Power, Leeds waalike Spurs ugani Elland Road nao Everton wakwaruzane na Bournemouth uwanjani Goodison Park. Everton wanashikilia nafasi ya 17 jedwalini kwa alama 33, mbili pekee kuliko Leicester na Leeds.

  • Tags

You can share this post!

Sipiganii tumbo langu, ninatetea mahasla – Raila

Mswada wachanganya Wabunge upande wa UDA

T L