• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
FWA yamtawaza beki Ruben Dias wa Manchester City Mchezaji Bora wa Mwaka 2020-21

FWA yamtawaza beki Ruben Dias wa Manchester City Mchezaji Bora wa Mwaka 2020-21

Na MASHIRIKA

BEKI Ruben Dias wa Manchester City ametawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka 2020-21 kwa upande wa wanaume kwenye tuzo zilizotolewa na Chama cha Waandishi wa Soka (FWA) mnamo Mei 20, 2021.

Sogora huyo raia wa Ureno mwenye umri wa miaka 24, alisajiliwa na Man-City kutoka Benfica kwa kima cha Sh9.1 bilioni mwishoni mwa msimu wa 2019-20 na akasaidia waajiri wake kutia kapuni taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na ubingwa wa Carabao Cup.

Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City walitinga pia nusu-fainali ya Kombe la FA na kwa sasa wanajiandaa kupepetana na Chelsea kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu.

“Ni staha kubwa kutuzwa. Bila shaka nisingepata tuzo hii bila ya ushirikiano mkubwa kutoka kwa wenzangu kikosini. Napongeza kikosi kizima cha Man-City kwa ukubwa na upekee wa mchango wao,” akasema Dias.

Dias aliwapiku Harry Kane wa Tottenham Hotspur na mwanasoka mwenzake kambini mwa Man-City, Kevin de Bruyne. Wanasoka tisa wa Man-City walikuwa wakiwania tuzo hiyo.

Dias ndiye mwanasoka wa tatu kutia kapuni taji hilo akicheza soka ya Uingereza kwa msimu wa kwanza. Beki wa mwisho kunyanyua ufalme huo ni Steve Nicol aliyekuwa mchezaji wa Liverpool miaka 32 iliyopita.

Mwanasoka matata wa Chelsea na timu ya taifa ya Uingereza, Fran Kirby alitawazwa mshindi wa tuzo hiyo ya FWA kwa upande wa wanawake.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Everton wakung’uta Wolves katika EPL na kujiweka...

Kaunti yatuma maafisa kuzima mzozo wa ardhi