• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 1:14 PM
Harambee Stars yawasili Morocco kuvaana na Mali inayoandamwa na majeraha

Harambee Stars yawasili Morocco kuvaana na Mali inayoandamwa na majeraha

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya Harambee Stars imewasili nchini Morocco huku wenyeji Mali wakisemekana huenda wakakosa huduma za wachezaji wanne timu hizi zitakapokabiliana ugani Agadir nchini Morocco hapo Oktoba 7.

Stars ya kocha Engin Firat iliondoka jijini Nairobi mnamo Jumatatu usiku na kuwasili Morocco mnamo Jumanne alasiri.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Mali, Cheick Doucoure (Lens, Ufaransa), Lassana Coulibaly (Salernitana, Italia) na Yves Bissouma (Brighton, Uingereza), wameumia.

Kiungo Doucoure aliumia kifundo dhidi ya Reims mnamo Oktoba 1. “Lens imethibitisha kujiondoa kwa mchezaji huyo wa kimataifa wa Mali,” gazeti la L’Essor lilisema Oktoba 5.

Coulibaly, ambaye pia ni kiungo, alijeruhiwa katika kipindi cha kwanza cha mechi ya Ligi Kuu nchini Italia dhidi ya Genoa mnamo Oktoba 2. “Alifanyiwa uchunguzi wa jeraha hilo hapo Oktoba 4 ambao ulifichua kuwa alichanika misuli. Kwa hivyo, kuna hofu kuwa huenda akakosa mechi zote mbili dhidi ya Kenya,” gazeti hilo liliongeza.

Kiungo Bissouma hajachezea Brighton tangu Septemba 19 alipoumia dhidi ya Leicester. “Kwa sasa, habari si nzuri kambini mwa Mali kwa sababu ya majeraha. Ilitarajiwa kuwa majeruhi hao watakuwa wamepona kabla ya mechi za kufa-kupona dhidi ya Kenya.”

Gazeti hilo linasema kuwa timu ya Mali maarufu kama Eagles ilianza kukusanyika jijini Agadir mnamo Oktoba 4 ilipokaribisha makipa Djigui Diarra (Young Africans, Tanzania) na Mohamed Niare (Stade Malien), kiungo Alou Dieng (Al Ahly, Misri) na mshambuliaji wa kati Adama Traore “Malouda” (Sheriff, Moldova).

Katika mechi hiyo ya Kundi E ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2022, kocha Mturuki Firat atawategemea wachezaji kama mshambuliaji Michael Olunga (Al Duhail, Qatar), kiungo Kenneth Muguna (Azam, Tanzania) na beki Joash Onyango (Simba SC, Tanzania).

Naye kocha Mohamed Magassouba atawategemea Hamari Traore (Rennes, Ufaransa), Falaye Sacko (Vitoria Guimaraes, Ureno), Diadie Samassekou (Hoffenheim, Ujerumani).

Mshambuliaji wa Mali, Kevin Lucien Zohi anayecheza nchini Ureno pia huenda akakosa mechi dhidi ya Kenya, lakini kutokana na stakabadhi za usafiri. Mali imekalia juu ya jedwali kwa alama nne ikifuatiwa na Kenya na Uganda (mbili kila moja) nayo Rwanda ni ya mwisho kwa alama moja.

You can share this post!

Viongozi wamwomboleza wakili Evans Monari

Nilimtusi Neymar, lakini si kwa ubaya – Mbappe