• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:55 AM
Nilimtusi Neymar, lakini si kwa ubaya – Mbappe

Nilimtusi Neymar, lakini si kwa ubaya – Mbappe

Na MASHIRIKA

KYLIAN Mbappe amekiri kwamba aliwahi kumtusi mwanasoka mwenzake kambini mwa Paris Saint-Germain (PSG), Neymar Jr.

Akihojiwa na kituo cha RMC Sport mnamo Oktoba 4, 2021 nchini Ufaransa, Mbappe, 22, aliungama kumfananisha Neymar na makalio. “Nilimtusi. Naam, nilimfananisha na makalio kwa kuwa hakutaka kunipa mpira uwanjani hata wakati nilipokuwa katika nafasi nzuri ya kufunga,” akasema.

Mechi iliyokuwa ikirejelewa na Mbappe ni ile ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) iliyokutanisha waajiri wake PSG na Montpellier mnamo Septemba 2021.

PSG walishinda mechi hiyo ya Ligue 1 dhidi ya Montpellier 2-0 na kupata motisha ya kusajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Manchester City katika Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

“Baada ya kutambua baadaye jinsi matusi hayo yalivyosambazwa mitandaoni, ilinilazimu kumzungumzia Neymar kuhusiana na kauli niliyotoa kumhusu,” akasema Mbappe kwa kukiri kwamba kuvurugika kwa uhusiano wake pia na Olivier kambini mwa Ufaransa huenda kukamchochea kuacha kuchezea timu hiyo ya taifa kwa muda.

“Tumebadilishana matusi mengi uwanjani. Ni kawaida kwa wanasoka kufanya hivyo kwa sababu ya mapenzi kwa timu na kiu ya kutaka kushinda mechi husika. Matusi mengine huchochewa na hasira ya kuona tunavyoelekea kupoteza mechi ambayo vinginevyo tungeshinda iwapo mwenzangu angenipa pasi ya kufunga bao,” akaeleza Mbappe.

“Hata hivyo, haina maana kwamba namdhalilisha Neymar kwa kumtusi. Namheshimu sana na ninamstahi kutokana na mafanikio yake kitaaluma,” akaongeza Mbappe.

“Nimekuwa katika ulingo wa soka kwa muda kiasi cha kufahamu kwamba ukweli wa jana haubadiliki kuwa uongo leo au hata kesho.”

“Iwapo ningeambiwa na mtu kwamba Lionel Messi angewahi kuja kuwa mwanasoka wa PSG, basi nisingeamini kabisa. Hivyo ukweli ni kwamba hakuna mchezaji ajuaye mustakabali wake kitaaluma. Mambo hutokea na mabadiliko hudumu,” akasema Mbappe.

“Kwa sasa mustakabali wangu si jambo ninalolipa kipaumbele. Tayari nimepoteza nguvu na muda mwingi wa kujibu tetesi za kila sampuli muhula huu. Hali hiyo ya kuandamwa mara kwa mara na maswali inachosha na kuchusha,” akaongeza sogora huyo anayehemewa pakubwa na Real Madrid.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Harambee Stars yawasili Morocco kuvaana na Mali...

Benki ya NCBA yazindua tawi la Ruiru