• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 AM
Harry Kane ataka Spurs wamwachilie atafute hifadhi mpya kwingineko mwishoni mwa msimu huu

Harry Kane ataka Spurs wamwachilie atafute hifadhi mpya kwingineko mwishoni mwa msimu huu

Na MASHIRIKA

FOWADI na nahodha Harry Kane amewaelezea waajiri wake Tottenham Hotspur kuhusu nia yake ya kuagana rasmi na kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mwishoni mwa msimu huu.

Tangazo hilo limechochea vikosi vya Manchester City, Manchester United, Chelsea na Barcelona kuanza kuyahemea maarifa ya supastaa huyo raia wa Uingereza.

Akihojiwa na Sky Sports mnamo Mei 17, 2021, Kane alifichua kwamba azma yake ni kusalia katika soka ya EPL japo alitaka masuala yote yanayofungamana na mustakabali wake kitaaluma kushughulikiwa na Spurs kabla ya kipute cha Euro 2021, ambacho Uingereza watashiriki, kuanza mnamo Juni 11.

Kane alisisitiza kwamba kubwa zaidi katika maazimio yake ni kujiunga na kikosi kitakachompa fursa ya kuanza kujitwalia mataji baada ya nafasi hiyo kukosekana kambini mwa Spurs ambao kwa sasa wanatiwa makali na kocha mshikilizi Ryan Mason.

Nyota huyo pia alieleza kwamba alilazimika kuahirisha mipango yake na kuguru Spurs miezi 20 iliyopita baada ya kuaminishwa kwamba waajiri wake wangalianza kujizolea mataji katika soka ya Uingereza na bara Ulaya baada ya mkufunzi Jose Mourinho kutua kikosini kuchukua mahali pa kocha Mauricio Pochettino ambaye kwa sasa anawatia makali masogora wa Paris Saint-Germain (PSG) nchini Ufaransa.

Yalikuwa matarajio ya Spurs msimu huu wa 2020-21 kukamilisha kampeni za EPL ndani ya orodha ya nne-bora na kutwaa ubingwa wa Carabao Cup. Hata hivyo, walisajili msururu wa matokeo duni kuanzia Disemba 2020 na wakashuka kutoka kileleni mwa jedwali. Aidha, kikosi hicho kilizidiwa maarifa na Man-City kwenye fainali ya Carabao Cup iliyowakutanisha mnamo Aprili 25, 2021.

Baada ya kumshawishi fowadi Edinson Cavani kurefusha mkataba wake ugani Old Trafford, Man-United wanasaka mshambuliaji atakayeshirikiana na kigogo huyo raia wa Uruguay. Kocha Ole Gunnar Solskjaer amedokeza mpango wa kumsajili chipukizi Erling Haaland wa Borussia Dortmund iwapo washindani watawapiku kwenye vita vya kuwania huduma za Kane anayemezewa pia na Real Madrid.

Mbali na Kane, Man-City wanawania pia maarifa ya wanasoka Haaland, Romelu Lukaku wa Inter Milan na Danny Ings wa Southampton.

Kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola kinamsaka fowadi atakayekuwa kizibo cha Sergio Aguero atakayeyoyomea Uhispania mwishoni mwa msimu huu kuchezea Barcelona. Chelsea pia wanavizia Haaland na Lukaku.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

RIZIKI: Kilimo cha miwa katika eneo la mimea inayochukua...

Idadi ya chini ya wapigakura yashuhudiwa eneobunge la Juja