• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
RIZIKI: Kilimo cha miwa katika eneo la mimea inayochukua muda mfupi kinampa tabasamu

RIZIKI: Kilimo cha miwa katika eneo la mimea inayochukua muda mfupi kinampa tabasamu

Na SAMMY WAWERU

KATIKA kijiji cha Gatumbiro, Ol Joro Orok, Kaunti ya Nyandarua Dison Wanjohi ni mkazi mwenye shughuli chungu nzima kwenye shamba lake lenye ukubwa wa ekari 20.

Kinachoifanya ratiba yake kuwa yenye matukio ainati, ni ukulima wa zao ambalo ni adimu Nyandarua.

Mzee Dison amejituma kukata kiu cha miwa kwa wenyeji eneo hilo.

Aidha, anakuza miwa eneo maarufu katika kilimo cha viazimbatata, mboga, mahindi, maharagwe na karoti, kati ya mimea mingineyo inayochukua muda mfupi kuanza kuvunwa.

Dison ametengea ekari moja ya shamba lake kuwa uga wa miwa.

“Mzee Dison ndiye mkulima wa kipekee Nyandarua anayekuza miwa kwa minajili ya kilimo-biashara,” asema, akiridhia jitihada zake.

Katika mazingira ya boma lake, miwa yenye urefu wa hadi urefu wa futi 10 itakukaribisha.

Hakuanza kilimo cha zao hilo hii leo, jana wala juzi. Ana zaidi ya miaka 14 katika uzalishaji wa miwa, tangu aache kazi ya udereva wa matrela.

Kabla kukumbatia kilimo cha miwa, Dison anasema alianza na matundadamu.

Kulingana na masimulizi yake, ukuzaji wa matunda hayo haukumpeleka alivyotarajia kwa kile anataja kama kukumbwa na changamoto chungu nzima.

“Nyandarua ni eneo lenye baridi, na matundadamu niliyopanda yalikuwa yakihangaishwa na ugonjwa wa ukungu, nikaamua kufanya utafiti wa mimea mingine ambayo ningelima,” asema.

Dison anasema alifanya utafiti wa kina, ulioishia kumshawishi namna angebadilisha taswira ya Nyandarua.

“Kaunti ya Nyandarua inajulikana sana kwa ukulima wa viazi, mboga, karoti, mahindi na maharagwe. Kimsingi, mimea inayochukua muda mfupi kuzalisha mazao.

“Utafiti niliofanya ulibaini kuwa ina hali bora ya anga na udongo kukuza miwa, tusiwe tunategemea mazao ya Kisii, Meru na pia Mumias,” anafafanua.

Hatimaye, alipata jawabu: “Nyandarua si tofauti na maeneo yanayofahamika kwa ukuzaji wa miwa”.

Kwa mujibu wa maelezo ya Dison, mwaka wa 2005 alitenga robo ekari kufanya jaribio.

“Nilitumia mtaji wa Sh10,000 pekee kuanza safari,” adokeza.

Mbegu, ambazo ni vipande vya miwa, alinununua kutoka Kisii na Meru. Mwaka mmoja na miezi sita hivi baadaye, mahesabu yake yaliingiana.

Utafiti aliozamia, na kuutekeleza kwa njia ya matendo ukabainisha Nyandarua si tofauti na Mumias, Meru na Kisii.

“Mazao ya kwanza nilitia kibindoni mapato yasiyopungua Sh15,000,” anasema.

“Niliongeza nusu ekari, nikawa nakuza miwa kwenye robo tatu. Kwa sasa nina jumla ya ekari moja,” anaongeza.

Cha kutia moyo katika kilimo cha miwa, Dison anasema gharama yake ni nafuu na ya chini mno ikilinganishwa na ukuzaji wa mimea inayochukua muda mfupi kuzalisha.

“Amini usiamini, mimea ninayoendelea kuvuna niliipanda miaka 10 na 15 iliyopita. Miwa ikipandwa, anachofanya mkulima ni kusubiri mazao,” anaelezea.

Miwa ni rahisi kupanda

Upanzi wa miwa, anasema huandaliwa mashimo yenye urefu wa futi mbili kuenda chini na upana wa kipenyo (diameter) cha futi mbili pia.

“Udongo wa juu, uliotolewa kwenye shimo unapaswa kuchanganywa na mbolea, kisha mchanganyiko huo urejeshwe shimoni. Bakisha inchi kama sita hivi kutunza miwa kwa maji na mbolea,” anasema.

Mkulima huyo alipanda miwa yake kwa kutumia mbolea ya mifugo; ng’ombe, mbuzi na kuku.

Nafasi kati ya mashimo na kwenye laini, ameipa futi sita.

Anasema kilimo chake ni hai, kisichotumia fatalaiza wala dawa zenye kemikali. “Ninaendelea kuridhia miwa niliyopanda zaidi ya miaka 10 iliyopita. Ninachofanya nyakati zingine, huifyeka ianze kumea upya,” anaiambia Taifa Leo.

Dison anasema changamoto za miwa ni haba mno. “Ninayoshuhudia ni miwa kukauka msimu wa baridi kali, kwa sababu ya barafu,” anasema.

Nyingine ni shambulizi la mdudu mdogo, anayesema akivamia mua huutoboa na kuugeuza rangi kuwa mweusi.

“Hutoboa shimo ndogo sana. Mua hugeuka kuwa mweusi na kuanza kukauka,” analalamika.

Mzee Dison Wanjohi akiwa katika shamba lake la miwa katika kijiji cha Gatumbiro, Ol Joro Orok, Kaunti ya Nyandarua. Picha/ Sammy Waweru

Boniface Kinyua, mtaalamu wa masuala ya kilimo, anasema mdudu huyo, funza wa mabua (stalk borer) anapodunga mua huufanya kuanza kuoza.

“Hugeuka rangi kwa sababu eneo lililotobolewa hupata kidonda, linaanza kuoza na hatimaye mua kukauka,” anafafanua mdau huyo ambaye pia ni meneja wa Tuko Fresh Farm, kampuni inayokuza aina tofauti ya stroberi na bukini.

“Kukabili funza wa mabua, mkulima amwagilie dawa ya wadudu hususan ile ya majimaji kwenye mashina ya mizizi ya miwa iliyoshambuliwa,” anashauri mtaalamu Kinyua.

Kimsingi, anasisitiza kilimo cha miwa hakina changamoto nyingi.

Wateja wa Mzee Dison ni wanunuzi rejareja, bei ya mua wenye urefu wa kati ya futi 6 – 10 ikiwa Sh30 – 40, bei ya langoni (farm gate price).

Vilevile, huuza kwa kukatakata vipande vidogo vya hadi Sh5. “Huwa sibagui ombi la mteja, Sh100 hazitakuwa kamilifu endapo zina upungufu wa Sh10,” anasema.

Huku lengo lake likiwa kubadilisha dhana ya Nyandarua, mkulima huyu anasema akipata wanunuzi wa jumla huenda atafanya maajabu.

“Kwa sasa ninakuza miwa kwenye ekari moja, kikwazo ni kupata soko la jumla. Nikipata wateja wanaonunua mazao yangu kwa malori, ninaapa kuongeza hadi zaidi ya ekari tano,” aeleza, akifichua shamba lake lina ukubwa wa ekari 20.

Hata ingawa ana sehemu aliyopanda matundadamu na mimea mingine, anasema shabaha yake ni kuona amebadilisha taswira ya Nyandarua.

“Si ajabu niibuke na kiwanda cha kuunda sukari na pia juisi ya miwa. Ninachoomba ni kupata idadi ya wanunuzi jumla wa kutosha,” asisitiza.

Ekari moja inakadiriwa kusitiri zaidi ya miwa 20, 000, na Dison anasema anapokamilisha kuvuna sehemu ya mwisho ya shamba lake, aliyotangulia huwa inaanza kubisha hodi kuingia sokoni.

You can share this post!

Ubelgiji kutegemea masogora tisa wa EPL kwenye fainali za...

Harry Kane ataka Spurs wamwachilie atafute hifadhi mpya...