• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
Huu ni mwaka wa Spurs kushinda mataji na wataanza kwa Carabao Cup – Mourinho

Huu ni mwaka wa Spurs kushinda mataji na wataanza kwa Carabao Cup – Mourinho

Na MASHIRIKA

KOCHA Jose Mourinho amesema ana kiu ya kushindia waajiri wake Tottenham Hotspur taji la kwanza chini ya ukufunzi wake msimu huu na fursa nzuri zaidi ya kufanya hivyo ni katika kampeni za League Cup.

Hata hivyo, amewataka masogora wake kutolegeza kamba wanapojifua kwa hatua ya nne-bora ya kivumbi hicho ikizingatiwa kwamba wapinzani wao Brentford watashuka dimbani kwa matarajio makuu ya kuwadengua.

Mourinho ni mshindi mara nne wa taji la Carabao Cup japo waajiri wake Tottenham hawajawahi kutia kibindoni ufalme wa kombe lolote tangu 2008.

Fainali ya Carabao Cup msimu huu wa 2020-21 imeratibiwa upya kutoka Februari 28 na sasa itasakatwa mnamo Aprili 25, 2021 uwanjani Wembley, Uingereza.

Mshindi wa kipute cha Carabao Cup msimu huu hatafuzu kwa Europa League kama ilivyokuwa awali. Badala yake, atafuzu kwa gozi la Uefa Europa Conference League ambalo ni shindano jipya kwenye soka ya bara Ulaya.

“Kosa litakalofanywa na wanasoka wa Spurs ni kuwabeza Brentford ikizingatiwa kwamba wapo baadhi ya wachezaji wangu walio na mazoea ya kupuuza kampeni za kuwania baadhi ya mataji,” akasema kocha huyo raia wa Ureno ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Inter Milan, FC Porto, Real Madrid, Chelsea na Manchester United.

Brentford wanaoshiriki Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Uingereza (Championship) watapepetana na Spurs huku mabingwa watetezi Manchester City wakitarajiwa kuvaana na Man-United kwenye nusu-fainali nyingine ya Carabao Cup msimu huu wa 2020-21.

Kinyume na misimu mingine ya awali ambapo michuano ya hatua ya nne-bora imekuwa ikitandazwa nyumbani na ugenini, mechi za muhula huu zitakuwa za mkondo mmoja pekee ili kuepuka mrundiko wa mechi baada ya kampeni za muhula huu kuchelewa kuanza kwa sababu ya corona.

Mechi hizo za nusu-fainali zimepangiwa kusakatwa kati ya Januari 4-6, 2021.

Man-United walifuzu kwa hatua ya nusu-fainali za Carabao Cup msimu huu baada ya kutandika Everton 2-0 kwenye robo-fainali mnamo Disemba 23, 2020 uwanjani Goodison Park.

Katika mechi ya awali iliyowakutanisha na Man-City ya kocha Pep Guardiola, Man-United waliambulia sare tasa mnamo Disemba 12, 2020 ugani Old Trafford.

Kwa upande wao, Man-City walitinga hatua ya nusu-fainali za Carabao Cup baada ya kuponda Arsenal 4-1 kwenye robo-fainali na watakuwa wakiwinda ubingwa wa taji hilo kwa mara ya nne mfululizo. Man-City waliwacharaza Man-United kwa jumla ya mabao 3-2 kwenye nusu-fainali za mikondo mikondo miwili mnamo 2019-20.

Spurs waliwapiga Stoke City 3-1 mnamo Disemba 23 na kujikatia tiketi ya kusonga mbele kwenye Carabao Cup muhula huu. Itakuwa mara yao ya kwanza tangu mwaka wa 2000 kukutana na Brentford waliofuzu kwa hatua ya nne-bora baada ya kuchabanga Newcastle United 1-0 mnamo Disemba 22, 2020.

NUSU-FAINALI ZA CARABAO CUP:

Manchester United na Manchester City

Tottenham Hotspur na Brentford

You can share this post!

Mwanamasumbwi Rayton Okwiri atemwa kwenye kikosi cha Hit...

Kinyang’anyiro cha kuwania taji la Koth Biro mwaka...