• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:07 PM
Ingwe yapigwa breki Ulinzi ikizidi kuzama

Ingwe yapigwa breki Ulinzi ikizidi kuzama

CECIL ODONGO na JOHN ASHIHUNDU

AFC Leopards jana Jumatatu walikosa kuendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Wazito kwenye mchuano uliosakatwa ugani MISC Kasarani.

Nairobi City Stars nao walizidisha masaibu ya Ulinzi Stars baada ya kuwachabanga 1-0, katika mechi nyingine iliyogaragazwa uga wa Ruaraka.

Ni ushindi uliofanya City Stars kuzidi kukwamilia nafasi ya tatu kwenye jedwali.

Kule Kasarani, Ingwe walichukua uongozi dakika ya tatu baada ya John Mark Makwatta kufunga mkwaju wa penalti.

Makwatta alikuwa ameangushwa katika eneo hatari na mnyakaji wa Wazito, Omar Adisa.

Hata hivyo, Wazito, ambao wanakodolewa macho na shoka la kushushwa ngazi, walikomboa dakika ya 62 kupitia nahodha Elly Asieche.

“Tumepata sare lakini tukapoteza nafasi kadhaa za kufunga. Leo Leopards wameponea japo nimeridhika na sare. Tuna matumaini ya kukwepa shoka jinsi wachezaji wanazidi kujituma kila mechi,” alisema kocha wa Wazito, Fred Ambani.

Sare hiyo iliacha Leopards katika nafasi ya 10 kwa alama 36 kutokana na mechi 25.

Wazito nao wapo namba 16 kwa alama 21 ikiwa imecheza mechi moja zaidi.

“Sina furaha kwa sababu leo tumecheza vibaya. Hata baada ya kufunga hatukuwa na msukumo wa kupata goli la pili, tukaruhusu Wazito kumiliki mpira. Katika kipindi cha pili tulilegea zaidi na hata mabadiliko hayakutusaidia,” alimaka Aussems akilaumu mabeki kuzembea.

Ugani Kasarani, nguvu mpya Oliver Maloba alifunga bao safi dakika ya 85 na kupalilia masaibu ya wanajeshi hao, ambao walizindua uga wa Ulinzi Sports Complex wiki jana.

Mshambuliaji wa Ulinzi, Masita Masuta, alikuwa amecheka na nyavu dakika ya 24 lakini bao lake likakataliwa kwa kuotea.

Ulinzi sasa haijashinda mechi sita mfululizo. Mara ya mwisho ilipozoa alama tatu ligini ilikuwa ushindi finyu wa 1-0 dhidi ya KCB, mnamo Februari 26 katika uga wa Kericho Green.

City Stars, maarufu kama ‘Simba wa Nairobi’ bado ni ya tatu kwa alama 45 zikiwa zimesalia mechi nane msimu ukamilike.

Wapo alama moja nyuma ya nambari mbili Tusker na alama tisa nyuma ya viongozi wa ligi Kakamega Homeboyz.

Ulinzi chini ya kocha Benjamin Nyangweso nao wapo katika nafasi ya 15 kwa alama 27 ikiwa na mechi mbili ambazo haijawajibikia.

Iwapo wataendelea kupigwa ligini, Ulinzi huenda ikapitwa na Wazito pamoja na Vihiga Bullets, ambao wanaonekana kuimarika na wanapigania kusalia ligini.

  • Tags

You can share this post!

Mafuriko: Watu 63 bado hawajajulikana waliko

CHARLES WASONGA: Idadi ndogo ya waliojitokeza mchujoni...

T L