• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mafuriko: Watu 63 bado hawajajulikana waliko

Mafuriko: Watu 63 bado hawajajulikana waliko

NA MASHIRIKA

DURBAN, AFRIKA KUSINI

IDARA za serikali nchini Afrika Kusini, jana Jumatatu zilisema kuwa zinaendelea kuwatafuta watu waliotoweka kufuatia mafuriko makubwa yaliyolikumba taifa hilo wiki iliyopita.

Hapo jana, idara hizo zilisema kuwa kufikia sasa, watu 63 hawajulikani waliko, huku 443 wakifariki.

Mafuriko hayo makubwa yalisababisha uharibifu mkubwa wa miundomsingi katika mkoa wa KwaZulu Natal.

Kulingana na taarifa zilizotolewa na idara mbalimbali, waokoaji wawili ni miongoni mwa watu waliofariki.

Tayari, serikali imeutaja mkoa huo kuwa eneo la hatari.

Kiongozi wa mkoa huo, Sihle Zikalala, alisema kuwa karibu makazi 4,000 yamesombwa na maji huku 8,000 yakiharibiwa.

Mengi ya makazi yaliyoharibiwa yako jijini Durban.

Polisi na waokoaji wamekuwa wakilazimika kutumia mbwa wa kunusa ili kuitafuta miili.Jumapili, polisi na jeshi walisema walipata miili sita zaidi.

Mwanamke mmoja, Lethiwe Sibiya, alisema kuwa bado hajampata mpwaye.

“Wakati maporomoko ya ardhi yalipotokea, alisombwa na maji. Hatujui aliko. Tumejaribu kuwarai polisi kufika katika eneo hili na mbwa wao lakini hatujafanikiwa,” akasema.

Mamlaka za serikali ilisema kuwa nyumba nyingi zilisombwa na mafuriko hayo kwani zilikuwa zimejengwa kwenye maeneo ya miinuko bila misingi thabiti.

Karibu shule na vituo vya afya 300 zimeharibiwa.

Baadhi ya wakazi wameachwa katika hali ya hatari, baada ya barabara na madaraja yanayoelekea kwenye makazi yao kuharibiwa kabisa.

“Hatuna umeme katika maeneo mengi,” akasema Imtiaz Syed, ambaye ndiye kiongozi wa vuguvugu la Active Citizens’ Coalition.

Alisema kuwa vuguvugu hilo linatathmini kuhusu njia linaloweza kutumia ili kuwasaidia waathiriwa kusafisha makazi yao na kupata maji safi ya kunywa.Serikali imekuwa ikielekezewa lawama kujenga upya barabara zilizoharibiwa na mafuriko hayo.

Zikalala alisema kuwa watu wanafaa kukoma kujenga makazi yao karibu na mito.

“Watu wengi bado wanakumbwa na hatari kubwa kwani wamejenga makazi yao karibu na mito. Kiukweli, hakuna jengo linalopaswa kuruhusiwa kujengwa karibu na mto,” akasema.

Kwenye ziara ya maeneo yaliyoathiriwa na janga hilo wiki iliyopita, Rais Cyril Ramaphosa alisema kuwa serikali yake “itafanya kila iwezalo kujenga upya miundomsingi iliyoharibiwa na kuzisaidia familia zilizoathiriwa na mafuriko hayo.”

Wataalamu wa hewa wanasema kuwa kuna uwezekano mkubwa mafuriko hayo yalichangiwa pakubwa na mabadiliko ya hali ya anga.

Ingawa kiwango cha mvua kimepungua, wanaonya kuwa hali ya hatari bado ingalipo.

“Hatujapoteza matumaini ijapokuwa tumekuwa na hofu kadri siku zinavyosonga,” akasema Sbongile Mjoka, ambaye ni mkazi wa kijiji cha Sunshine, eneo la Thekwini.

Mpwa wake wa miaka minane ni miongoni mwa watu ambao hawajulikani waliko.

  • Tags

You can share this post!

Mithika Linturi ateua mgombeaji mwenza

Ingwe yapigwa breki Ulinzi ikizidi kuzama

T L