• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Jesse Were asherehekea kufikisha mabao 100 Zesco United baada ya kutinga “hat-trick”

Jesse Were asherehekea kufikisha mabao 100 Zesco United baada ya kutinga “hat-trick”

Na GEOFFREY ANENE

TEGEMEO Jesse Jackson Were alifikisha idadi ya mabao amefungia Zesco United tangu ajiunge nao kuwa 100 baada ya kufuma wavuni mabao matatu wakipepeta Kitwe United 4-0 kwenye Ligi Kuu ya Zambia mjini Ndola, Jumapili.

Mshambuliaji Were,32, alijiunga na Zesco mnamo Januari 1, 2016 akitokea Tusker FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya. Hii ilikuwa wiki chache baada ya kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Kenya 2015 kwa kutikisa nyavu mara 22.

Mshindi huyo wa Ligi Kuu ya Kenya mwaka 2012 akiwa Tusker, amechezea Zesco jumla ya mechi 27 kwenye Klabu Bingwa Afrika, nane katika Kombe la Mashirikisho la Afrika pamoja na nyingine nyingi katika mashindano mbalimbali ya Zambia.

Katika michuano ya Afrika, mshikilizi huyo wa rekodi ya mchezaji aliyefungia Zesco mabao mengi katika historia ya klabu hiyo, amechangia magoli 12 pamoja na kusuka pasi mbili zilizozalisha mabao.

Were, ambaye anajivunia kushinda Ligi Kuu ya Zambia mwaka 2017, 2018 na 2019, amechezea timu ya taifa ya Kenya ya Harambee Stars mara tisa.

Zesco, ambayo pia imeajiri Wakenya kipa Ian Otieno na mshambuliaji John Makwata, inaongoza ligi ya msimu 2020-2021 kwa alama 61 kutokana na michuano 30.

Katika ligi hiyo ya klabu 18, Zanaco ni ya pili kwa alama 53 nayo Kabwe Warriors inafunga mduara wa tatu-bora kwa pointi 47. Zanaco na Kabwe zimesakata mechi 31 kila moja.

Lusaka Dynamos anayochezea kiungo Duncan Otieno na beki Musa Mohammed, ni ya sita kwa alama 46.

Nkana anayochezea kiungo Duke Abuya na NAPSA Stars ambayo imeajiri beki David Owino na kipa Shaaban Odhoji, zinapatikana katika mduara hatari wa kutemwa katika nafasi ya 15 na 16 zikiwa zimezoa alama 37 na 36, mtawalia.

You can share this post!

Chelsea tayari kumsajili Romelu Lukaku kutoka Inter Milan

COPA AMERICA: Kiungo James Rodriguez atemwa kwenye kikosi...