• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Chelsea tayari kumsajili Romelu Lukaku kutoka Inter Milan

Chelsea tayari kumsajili Romelu Lukaku kutoka Inter Milan

Na MASHIRIKA

CHELSEA wako tayari kumsajili upya mshambuliaji matata raia wa Ubelgiji, Romelu Lukaku huku kocha Thomas Tuchel akifichua kwamba malengo yake ni kunyanyulia wafalme hao wa bara Ulaya taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu ujao wa 2021-22.

Tuchel amesema Chelsea almaarufu ‘The Blues’ wanahitaji fowadi mpya atakayeshirikiana vilivyo na Timo Werner, Christian Pulisic na Kai Havertz katika safu ya mbele na sogora ambaye yeye anahisi kwamba ana uwezo wa kutambisha zaidi kikosi hicho ni Lukaku wa Inter Milan.

Baada ya kusuka kikosi kinachojivunia masogora stadi katika safu ya ulinzi, mafowadi wa Chelsea wamefunga zaidi ya mabao mawili mara moja pekee kutokana na mechi 30 zilizopita ambazo zimesimamiwa na Tuchel.

Licha ya Lukaku kufungia Inter jumla ya mabao 33 kwenye Ligi Kuu ya Italia na kuzolea kikosi hicho taji la kipute hicho, Inter wako radhi kumtia sogora huyo mnadani ili kupunguza gharama ya matumizi ya fedha.

Kwa mujibu wa Tuchel, maamuzi ya kuwania huduma za Lukaku yanachochewa na kudidimia kwa matumaini ya Chelsea kujinasia maarifa ya nahodha wa Tottenham Hotspur, Harry Kane ambaye pia anaviziwa na Manchester City na Manchester United.

Chelsea wanamhemea pia fowadi chipukizi raia wa Norway, Erling Haaland. Hata hivyo, wanakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Man-City wanaotafuta kizibo cha Sergio Aguero ambaye tayari ameafikiana na Barcelona kutua ugani Camp Nou.

Baada ya kujiunga na Chelsea akiwa na umri wa miaka 18 pekee mnamo 2011, Lukaku aliwajibishwa mara moja pekee kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kabla ya kutumwa kwa mkopo kuchezea West Bromwich Albion na Everton ambao hatimaye walimsajili kwa kima cha Sh3.9 bilioni mnamo 2014.

Lukaku kwa sasa anachukuliwa kuwa miongoni mwa mafowadi mahiri zaidi katika soka ya bara Ulaya na Inter wamefichua kwamba kikosi chochote kinachowania maarifa ya sogora huyo kitalazimika kuweka mezani kima cha Sh14 bilioni.

Mbali na fowadi, Chelsea wamefichua mpango wa kumsajili pia kiungo mbunifu na beki mmoja. Miongoni mwa viungo wanaohusishwa na kikosi hicho ni Declan Rice wa West Ham United.

Callum Hudson-Odoi anayemezewa mate na Borussia Dortmund pamoja na Tammy Abraham, Billy Gilmour, Olivier Giroud na Fikayo Tomori ni miongoni mwa wanasoka wanaotarajiwa kuagana rasmi na Chelsea mwishoni mwa Juni 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mashamba bado donda sugu Kenya kwa miaka 58 ya uhuru

Jesse Were asherehekea kufikisha mabao 100 Zesco United...