• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:50 AM
Jinsi mpishi kutoka Kenya anavyotekeleza wajibu muhimu katika klabu ya Arsenal

Jinsi mpishi kutoka Kenya anavyotekeleza wajibu muhimu katika klabu ya Arsenal

NA RUTH AREGE

MPISHI mzaliwa wa Kenya Bernice Kariuki mwenye umri wa miaka 51, ambaye alizaliwa katika eneo la Ofafa Jericho jijini Nairobi, ameiweka Kenya kwenye ramani ya juu duniani kwa kuwa mpishi wa kikosi cha kwanza cha klabu ya Arsenal ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Kariuki, ni miongoni mwa wapishi 90 wa klabu hiyo ambao huwapikia wachezaji hao. Kikosi cha kwanza cha Arsenal kina wapishi 27.

Kitu ambacho wengi hawakijui ni kuwa, klabu ya Arsenal inawachezaji 25 na kila mchezaji anampishi wake binafsi.

Wachezaji hawa wanakula vyakula tofauti tofauti kulingana na jinsi mtaalamu wa lishe anavyo agiza. Hili linawasaidia wachezaji kutoongeza uzito ambao utawatatiza wanapocheza.

Timu nzima ya Arsenal ina wachezaji 118 ambao wanacheza soka ya kulipwa, idadi hiyo haijajumuisha wakufunzi na benchi la ufundi.

Kikosi hicho kimejumuishwa timu ya wanawake inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake ya (EWPL) na pia akademia ya wanawake na wanaume.

Mpishi huyo wa zamani wa klabu ya Tottenham ya EPL, amefanya kazi hii kwa miaka 15. Anasema pia amewahi kuipikia Familia ya Kifalme ya Uingereza.

Akizungumza na Chams Media katika runinga ya NTV siku ya Jumamosi alisema, kukutana na  nahodha wa zamani wa Arsenal ambaye kwa sasa anaipigia timu ya Chelsea ya EPL Pierre Emireck Aubameyang, kulibadilisha maisha yake hadi sasa.

“Kuna wakati nilikuwa kwenye sherehe moja ya krismasi na Aubameyang alikuwepo. Nilipata muda wa kuongea naye na nilimuliza ikiwa naweza pata kazi ya upishi kwenye klabu ya Arsenal. Moja kwa moja alinipa kazi niwe mpishi wake wa ndani. Alipenda nilivyo pika pilau kwenye sherehe hiyo. Hiki ni chakula ambacho alikipenda sana ingawa hakujua mimi ndiye nilikipika,” alisema Kariuki.

Aidha anasema, anafanya kazi saa14 kwa siku, saa 90 kwa wiki ambapo zamu yake huanza asubuhi mwendo wa saa 9:00 asubuhi.

“Kazi yetu huanza saa 9:00 asubuhi. Tunaanza kwa kupika samaki kwa kuwa wachezaji wengi wanapenda sana samaki. Ifikapo saa 10:00 asubuhi, wachezaji  huwa wameamka kujiandaa kwa mazoezi ya kukimbia. Kabla kuingia mazoezini, tunawaandalia sharubati na maziwa baridi yaani ‘Milk Shake’. Wakimaliza kukimbia wanapata kiamsha kinywa halafu wanarudi kupumzika, ifikapo saa saba mchana wanarudi tena mazoezini,” aliongezea Kariuki.

Hata hivyo anasema, yuko tayari kuanza mafunzo ya upishi hapa nchini kwa wanafunzi ambao wanataka kusomea upishi.

“Kwa sasa tuko na serikali mpya, na rais wetu ni mchapa kazi. Tunaweza kufanya kazi pamoja kwa sababu mimi ni mchapa kazi pia. Tuna wapishi wazuri nchini lakini hawajiamini kwa kazi yao. Ni wakati sasa wapishi Wakenya waamke tuanze kutimiza na kujenga ndoto zetu,” alisema Kariuki.

  • Tags

You can share this post!

Rigathi ataka Raila, Kalonzo waipe serikali ya Kenya Kwanza...

Juventus yajinyanyua dhidi ya Torino na kupunguzia kocha...

T L