• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Rigathi ataka Raila, Kalonzo waipe serikali ya Kenya Kwanza muda zaidi kabla ya kuikosoa

Rigathi ataka Raila, Kalonzo waipe serikali ya Kenya Kwanza muda zaidi kabla ya kuikosoa

NA CHARLES WASONGA

NAIBU Rais Rigathi Gachagua sasa anawataka viongozi wa upinzani wakome kuikosoa serikali ya Kenya Kwanza bali waipe muda zaidi irekebishe makosa ambayo wao (upinzani) walitenda kwa miaka mitano.

Akiongea Jumapili, Oktoba 16, 2022  wakati wa ibada ya kutoa shukrani iliyofanyika katika uwanja wa michezo wa Kericho Green, kaunti ya Kericho, Bw Gachagua amesema hawawezi kurekebisha makosa ya kiuchumi ya serikali ya Jubilee kwa siku tatu pekee.

“Mtupe muda tusafishe makosa ambayo mlifanya kwanza kabla ya ninyi kutathmini utendakazi wetu. Baada ya hapo ndio itakuwa sawa kwenu kutukosoa. Siku 30 hazitutoshi kukarabati uchumi ambao mliharibu na kuwaletea Wakenya mahangaiko wanayopitia sasa,” akasema Bw Gachagua.

Hata hivyo, Naibu Rais hakusema ni lini watamaliza kurekebisha makosa ya kiuchumi yaliyosababishwa na utawala wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, ambaye alishirikiana kisiasa na kiongozi wa ODM Raila Odinga wakati wa muhula wake wa pili uongozini.

Bw Gachagua amesisitiza kuwa yeye na Rais William Ruto walirithi uchumi ulioporomoka akisema kuwa wameanza kuukarabati kwa kupunguza gharama ya uzalishaji chakula, kupitia upunguzwaji wa bei ya mbolea.

“Vile vile, tumeanza kuhakikisha kuwa asasi za serikali zinaruhusiwa kuendesha majukumu yao kwa njia huru bila kuingiliwa na wanasiasa. Tumewahakikishia polisi na machifu kwamba hawatatumika kuendesha siasa jinsi ilivyokuwa katika serikali iliyopita. Aidha, tumewaambia Makamishna wa Kaunti kuachana na siasa na wahudumie Wakenya kwa usawa,” akaeleza.

“Aidha, tumejitolea kuhakikisha kuwa pesa ambazo zinakusanywa na Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) zinatumika kufadhili miradi ya maendeleo na hazielekezwi ndani ya mifuko ya watu,” Bw Gachagua akaongeza.

Naibu Rais alionekana kuwajibu vinara wa Azimio Raila Odinga na Kalonzo Musyoka ambao wamekuwa wakiikosoa kwa kile wanachosema ni kutotimiza ahadi ya kupunguza gharama ya maisha.

You can share this post!

Msukosuko wachemka katika Azimio

Jinsi mpishi kutoka Kenya anavyotekeleza wajibu muhimu...

T L