• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Kane, Son waandika historia

Kane, Son waandika historia

WASHAMBULIAJI Harry Kane na Son Heung-min waliandikisha historia Jumatano usiku baada ya kuona lango Tottenham Hotspur wakipepeta wenyeji Crystal Palace 4-0.

Wawili hao wamefunga magoli 34 pamoja kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), wakifuta rekodi ya awali iliyoshikiliwa na Mohamed Salah na Sadio Mane kutoka Liverpool. Mane aliondoka Liverpool mwisho wa msimu uliopita.

Wachache walitarajia magoli mengi kati ya Spurs na Palace baada ya wenyeji kudhibiti pakubwa kipindi cha kwanza ugani Selhurst Park.

Hata hivyo, Spurs ya kocha Antonio Conte ilitoa kucha zake kali kwa kumiminia Palace mabao mawili ndani ya dakika nane za kwanza kupitia kwa Kane.Matt Doherty aliongeza bao la tatu dakika ya 68.

Son alihitimisha dakika chache baadaye alipopata bao lake la kwanza ligini tangu ‘hat-trick’ dhidi ya Leicester mnamo Septemba 17.

Bao hilo lilitosha kuingiza Son na Kane katika daftari za kumbukumbu kama wachezaji wawili waliopata mabao mengi pamoja kuliko wote kwenye EPL. Son alieleza baada ya mechi kuwa alisikitika kuwa hajasaidia timu yake pakubwa katika kampeni za msimu huu.

“Hapa ni mahali pagumu kupata pointi. Hata hivyo, tulistahili ushindi. Tulidhibiti mchezo katika kipindi cha pili na kupata magoli manne matamu. Nilikuwa nimesubiri kwa muda mrefu bao hili! Nilihisi vizuri sana. Nasikitika kuwa sijakuwa nikipata mabao kwa sababu najua matarajio ya wenzangu kwangu ni makubwa. Natumai leo ni mwanzo mpya, kupata kujiamini tena na nitaendelea kusaidia timu,” aliongeza.

Kane, ambaye anahitaji mabao mawili kufikia rekodi ya Jimmy Greaves ya kufungia Spurs mabao 266, sasa yuko makini kuendeleza ukatili wake baada ya pigo dhidi ya Aston Villa hapo Januari 1.

Aidha, Conte ameonywa na wachanganuzi dhidi ya kutaka Spurs imwage fedha nyingi sokoni kununua wachezaji katika kipindi hiki kifupi cha uhamisho. Wanasema hii inaweza kuchochea wachezaji alionao kutojituma kwa kuona kuwa hana imani nao. Wakati huo huo, Spurs inasemekana iko tayari kuanzisha mazungumzo na Kane ya kuimarisha kandarasi yake.

Spurs inakamata nafasi ya tano. Itavaana na majirani Arsenal katika mchuano ujao mnamo Januari 15.

Matokeo ya EPL (Januari 4):

Southampton 0 Nottingham Forest 1

Leeds 2 West Ham 2

Aston Villa 1 Wolves 1

Crystal Palace 0 Tottenham Hotspur 4

  • Tags

You can share this post!

DOMO: Huyu Syokau atatoboa?

Zukini na faida za kuila

T L