• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
Kenya ilivyozoa medali 6 taekwondo Afrika 2021 Ogalo akishiriki Olimpiki

Kenya ilivyozoa medali 6 taekwondo Afrika 2021 Ogalo akishiriki Olimpiki

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Nesmas Wesonga anaamini kuwa taekwondo ndio mchezo maarufu wa miereka nchini Kenya kutokana na wachezaji wa fani hiyo walivyofanya mashindanoni 2021.

Wesonga, ambaye amefundisha na kukuza talanta ya taekwondo kwa miaka 29, anaipa timu ya Kenya alama sita kwa 10 ilivyofanya kimataifa mwaka 2021 ulioshuhudia Kenya ikirejea kwenye Olimpiki baada ya miaka 13 kupitia kwa Faith Ogalo.

“Kwa mara ya kwanza kabisa katika historia yetu tulipata kushiriki mashindano manne makubwa ambayo ni; mashindano ya Afrika mwezi Machi jijini Dakar nchini Senegal, Olimpiki mwezi Julai/Agosti jijini Tokyo nchini Japan, mashindano ya taekwondo ya dunia ya walemavu jijini nchini Uturuki mwezi Desemba na Senegal International Open jijini Dakar, Senegal mwezi Desemba,” anasema.

Matokeo mazuri ya Kenya katika mashindano hayo manne yalipatikana jijini Dakar mwezi Desemba.

Mwanaolimpiki wa kwanza kabisa Milka Akinyi, ambaye alishiriki Olimpiki 2008 jijini Beijing, Uchina, alizoa medali ya dhahabu kwenye Senegal Open katika uzani wa “Light”.

Sharon Nafula pia alinyakua dhahabu katika uzani wa Bantam nao Mary Muriu (Feather) na Doreen Matekwa (Welter) wakaridhika na nishani za fedha katika vitengo hivyo vyao.

Wachezaji wa timu ya taifa ya chipukizi kutoka kushoto; Pauline Zawadi (Light middle) kocha George Muriu, Mary Wanjiru (Flyweight) na Shadia Mebora (Bantamweight) wakiwa katika chuo cha Taekwondo Academy awali. PICHA | MAKTABA

Mwanaolimpiki wa pili mwanamke kutoka Kenya, Faith Ogallo, ambaye alikuwa jijini Tokyo, Japan, mwezi Julai/Agosti, alishinda medali ya shaba katika mashindano ya Afrika katika uzani wa “Heavy” jijini Dakar, wakati ambao pia Everlyn Aluoch alizoa shaba katika uzani wa “Welter”.

“Bila shaka, tulipiga hatua kubwa mbele katika taekwondo yetu mwaka 2021. Naamini mchezo huu wa miereka umepata umaarufu zaidi hapa nchini, hasa kwa watoto wanaoenda shule,” anasema.

Mwaka 2022 utakuwa wa shughuli nyingi kwa wanataekwondo.

Kwa mujibu wa Wesonga, Kenya inapanga kushiriki mashindano ya dunia ya kyorugi nchini Uchina, mashindano ya dunia ya poomse nchini Korea Kusini na mashindano ya chipukizi nchini Botswana, miongoni mwa mengine.

Tofauti na kinadada wa Kenya waliosherehekea matokeo mema, wachezaji wenzao wanaume hawakushinda medali yoyote katika mashindano ya kimataifa.

“Sababu za wanaume kufanya vibaya ni kuwa taekwondo ya wanaume ilianza mapema duniani na ina ushindani mkali. Pia, kinadada wetu wanaolelewa katika mazingira magumu wanapata kujifunza mchezo huu na kuwa na misuli inayohitajika. Kazi za nyumbani pia zinawasaidia kuwa na nguvu wanapokuwa. Kwa upande wa wanaume, lazima pia tukubali kuwa tunahitaji kuwekeza zaidi katika mafunzo ya muda mrefu ya kisayansi ili kufika kiwango cha kushinda medali,” Wesonga anasema.

Wesonga anasema kuwa kuna matumaini makubwa katika mchezaji Newton Maliro kutoka jeshi la KDF (uzani wa Heavy), Innocent Wafula kutoka Chuo Kikuu cha Kibabii (uzani wa kati) na Shawn Michael Ochieng kutoka Chuo Kikuu cha Strathmore.

“Wameshiriki mashindano kadhaa ya kimataifa kwa hivyo wana ujuzi,” afisa huyo anasema.

You can share this post!

Salah, Elneny na Trezeguet kuongoza Misri katika fainali za...

GWIJI WA WIKI: Geoffrey Mwamburi

T L