• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
Kenya kunufaika na kuchaguliwa kwa Maluki kuwa mwenyekiti wa Judo Afrika

Kenya kunufaika na kuchaguliwa kwa Maluki kuwa mwenyekiti wa Judo Afrika

Na GEOFFREY ANENE

KENYA na eneo la Afrika Mashariki na Kati zitanufaika pakubwa na kuchaguliwa kwa raia wake Shadrack Maluki kuwa mwenyekiti wa Shirikisho la Judo Afrika (AJU) kwenye uchaguzi wa Mei 18 mjini Casablanca nchini Morocco.

Maluki alidokeza kuwa uwezekano wake wa kuchaguliwa kuongoza shirikisho hilo utawezesha kufikiwa na miradi ya AJU na Shirikisho la Kimataifa la Judo (IJF).

“Tutakuwa na usemi katika kuendesha shughuli za bara na pia wachezaji wetu wa judo kunufaika zaidi na udhamini na mafunzo ya hali ya juu,” alisema Maluki na kuongeza kuwa makocha na wasimimazi wa mechi pia watapata kozi za kuwaimarisha.

Maluki, ambaye pia ni naibu wa kwanza wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki Kenya (NOC-K), alisema kuchaguliwa kwake pia kutaharakisha ujenzi wa kituo cha maendeleo cha AJU na kuandaliwa kwa mashindano ya haiba ya Grand Slam jijini Nairobi.

Maluki alikuwa akizungumza katika siku ya mwisho ya mkutano wa mashauriano wa siku mbili hapo Machi 28 wakati wagombea wengine walitumia fursa hiyo kujipigia debe kwa nyadhifa tofauti.

Wajumbe 25 kutoka mataifa 25 walihudhuria mkutano huo akiwemo mwenyekiti wa sasa wa AJU, Thierry Siteny kutoka Madagascar, ambaye atatetea taji lake la AJU mwezi Mei.

“Tumesalia nyuma katika judo kwa sababu nguvu zote zimekuwa zikielekezwa katika mataifa ya Kaskazini na Magharibi mwa Afrika na hali hiyo itabadilika,” alisema Maluki.

Alifichua kuwa Kenya huenda ikaandaa mashindano ya Grand Slam yatakayofahamika kama Safari Judo Grand Slam baadaye mwaka huu ikiwa visa vya ugonjwa wa Covid-19 vitakuwa vimepungua na kuongeza kuwa wako katika harakati ya kutafuta shamba katika kituo cha kimataifa cha michezo cha Kasarani kufanikisha ujenzi wa kituo cha judo.

Kikifaulu, kituo hicho kitakuwa cha pili barani Afrika baada ya kile cha Casablanca, Morocco ambacho ujenzi tayari unaendelea na unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi mitatu.

Mashindano ya Grand Slam ni ya tatu kwa fahari katika michezo ya judo duniani baada ya Olimpiki na mashindano ya dunia.

Miji mingine mitano inayoandaa Grand Slams ni Antalya (Uturuki), Paris (Ufaransa), Tashkent (Uzbekistan), Tbilisi (Georgia) na Tel Aviv (Israel).

“Tumeshazungumza na Wizara ya Michezo na tunapitia baadhi ya vitu vinavyohitajika kufanywa kisheria kabla tupokee shamba hilo rasmi,” alieleza Maluki. “Tungependa kushukuru Siteny na AJU kuchagua Nairobi kuwa mwenyeji wa Grand Slam na pia kituo cha maendeleo. Ni heshima kubwa.”

Siteny alisema kuwa kikosi kitaundwa mara mkutano wa mwaka utakamilika nchini Morocco kushughulikia njia zitakazohakikisha shindano la Grand Slam jijini Nairobi linafaulu.

  “Haitakuwa tu kuhusu Kenya, lakini Afrika kwa sababu Grand Slam itakuwa inakuja Afrika kwa mara ya kwanza kabisa,” alieleza Siteny na kuongeza kuwa Kenya na Afrika zina uwezo wa wa kuandaa mashindano makubwa kama hayo yanayovutia mataifa 160.

  • Tags

You can share this post!

Kampuni za ndege Afrika zakumbatia teknolojia ya paspoti za...

Wavamiwa na nyuki baada ya kuiba mtungi wa gesi na...