• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Kenya kusaka leo tiketi ya Kombe la Dunia la walemavu

Kenya kusaka leo tiketi ya Kombe la Dunia la walemavu

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya Kenya itakuwa mawindoni hii leo Jumatano kwenye robo-fainali ya Kombe la Afrika soka ya walemavu (CANAF), jijini Dar es Salaam, Tanzania, kutafuta tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia 2022.

Vijana wa kocha Willis Odhiambo walipoteza mchuano wao wa mwisho wa Kundi B dhidi ya mabingwa wa dunia Angola, kwa kichapo cha mabao 3-0 uwanjani Jakaya Mrisho Kikwete, Jumanne.

Hata hivyo, Kenya tayari ilikuwa imejikatia tiketi ilipokung’uta Zanzibar 5-0 siku ya Jumatatu.

Nambari mbili wa Kundi B Kenya watavaana na mshindi wa Kundi D, aliyetarajiwa kufahamika baadaye jana Jumanne kutoka orodha ya Ghana, Nigeria na Misri.

Timu zote zitakazoingia nusu-fainali zitanyakua tiketi ya kuelekea nchini Uturuki mwezi Oktoba 2022 kushiriki Kombe la Dunia.

Mnamo Jumanne, nahodha Dalmas Otieno alishutumu refa wa mchuano dhidi ya Angola akisema “aliwaua”.

“Refa wa kupuliza kipenga alitupatia penalti tena akatupokonya,” alisema Otieno na kukiri pia kuwa Kenya inastahili kuimarisha ulinzi wake pamoja na kurekebisha makosa kutoka kwa kipa.

Angola, ambayo ililemea Uturuki katika fainali ya Kombe la Dunia 2018 kwa njia ya penalti, ilizamisha Kenya kupitia mabao ya Sabino Joaquim, Joao Chiquete na Hilario Kufula.

Tanzania maarufu kama Tembo Warriors na Morocco pia waliingia robo-fainali hapo jana.Warriors walilemea Sierra Leone 1-0 nao Morocco wakapepeta Uganda Cranes 3-1.

Mataifa mengine yaliyoinia mashindano hayo ni Cameroon, Liberia na Gambia (Kundi C). Kenya imenogesha Kombe la Dunia mwaka 2014 na 2018 nchini Mexico.

Ilishindwa kusonga mbele kutoka Kundi C mjini Culiacan mwaka 2014.Ilirejea mnamo 2018 lakini ilibanduliwa katika hatua ya 16-bora mjini San Juan de los Lagos.

  • Tags

You can share this post!

BALLON D’OR: Messi tena? Lewandowski kachezwa!

MAKAVAZI CUP: Omariba, Sakawa waibuka mabingwa wa vishale

T L