• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:35 AM
Kipa Hugo Lloris wa Ufaransa astaafu soka ya kimataifa

Kipa Hugo Lloris wa Ufaransa astaafu soka ya kimataifa

Na MASHIRIKA

KIPA wa timu ya taifa ya Ufaransa, Hugo Lloris, ametangaza kustaafu soka ya kimataifa akiwa na umri wa miaka 36.

Nahodha huyo wa Tottenham Hotspur anafikia uamuzi huo wiki tatu baada ya Ufaransa kufungwa penalti 4-2 na Argentina kwenye fainali ya Kombe la Dunia nchini Qatar mnamo Disemba 18, 2022.

Lloris aliyekuwa nahodha wa Ufaransa, alikuwa ameongoza taifa hilo kunyanyua ubingwa wa Kombe la Dunia mnamo 2018 baada ya kupepeta Croatia 4-2 nchini Urusi.

“Nimeamua kutia breki safari yangu ya soka ya kimataifa nikihisi kwamba nimejituma vilivyo katika kipindi kizima ambapo nimewajibikia Ufaransa,” akasema Lloris katika mahojiano yake na gazeti la L’Equipe.

“Nahisi kwamba imekuwa vyema nitangaze uamuzi huo miezi miwili na nusu kabla ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa mechi za kufuzu kwa fainali za Euro kuanza,” akaongeza Lloris.

Ufaransa wametiwa katika kundi moja na Gibraltar, Ugiriki, Uholanzi na Jamhuri ya Ireland katika michuano hiyo ya kufuzu kwa fainali za Euro 2024.

Lloris alianza kutandaza soka kambini mwa Ufaransa akiwa na umri wa miaka 21 na aliwajibishwa dhidi ya Uruguay katika pambano la kirafiki mnamo Novemba 2008.

Mechi ya fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Argentina nchini Qatar ilikuwa yake ya 145 na ndiye mwanasoka anayejivunia rekodi ya kuwajibikia Ufaransa katika michuano mingi zake.

Amevalia utepe wa unahodha kambini mwa Ufaransa mara 121 ambayo pia ni rekodi mpya.

Lloris anaangika glavu zake kimataifa siku chache baada ya kocha Didier Deschamps kurefusha kandarasi yake kambini mwa Ufaransa hadi Juni 2026.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Sote tuunge mkono nia ya mapatano ya Rais Ruto

WANDERI KAMAU: Mwanadamu amegeuka mnafiki asiyesameheka!

T L