• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 5:45 AM
TAHARIRI: Sote tuunge mkono nia ya mapatano ya Rais Ruto

TAHARIRI: Sote tuunge mkono nia ya mapatano ya Rais Ruto

NA MHARIRI

TANGU jadi pindi uhuru ulipopatikana, siasa za Kenya zilianza kuchukua mkondo wa kikabila.

Chuki za kikabila zimekuwa zikifufuliwa na kufikia kilele katika kipindi cha uchaguzi mkuu.

Wanasiasa wengi, hasa wanaowania urais, ndio wamekuwa katika mstari wa mbele katika uovu wa kuvuvia ukabila miongoni mwa Wakenya.

Kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017, aliyekuwa rais wa Amerika, Barack Obama alishangaa ni vipi wanasiasa wanaowagawanya wananchi kwa cheche za kikabila wakati wa kampeni, watakavyorejesha umoja wa kitaifa watakapotwaa mamlaka.

Wakati huo wawaniaji wakuu wa urais walikuwa rais mstaafu Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM, Raila Odinga. Walikuwa wameipasua Kenya katikati kutokana na matamshi yao yasiyoadilifu.

Bw Uhuru alimuita Raila Muguruki na Kimudu inayofasiriwa kama mwendawazimu na jitu mtawalia, huku Raila akimrejelea Uhuru kama mlevi na naibu wake Dkt William Ruto kama mwizi.

Kwa kutumia maneno hayo machafu, Bw Uhuru na Ruto walilenga kuvutia hasa wapigakura wa Mlima Kenya na wa jamii ya Wakalenjin, hali ambayo kwa upande mwingine iliamsha chuki kubwa miongoni mwa Wakenya.

Waama, haikuchukua muda mrefu kabla ya Uhuru kubaini uhalisia wa kauli ya Obama. Katika juhudi za kurejesha amani nchini, baada ya kuchaguliwa rais 2017, alipatana na Raila. Lakini kwa bahati mbaya, naibu wake, Dkt Ruto, alionekana kutofurahia hilo.

Alianza kampeni kali za kumsawiri Uhuru kama aliyepotoshwa na Raila. Kwa kufanya hivyo, alifanikiwa kuhifadhi ngome zote za Uhuru pamoja na kunyofoa maeneo kadhaa ambayo yalimshabikia Raila.

Lakini jinsi walivyosema wahenga muwi huwa mwema, kwa sasa Rais Ruto ameghairi maazimio yake na kuanza mikakati ya kuunganisha nchi. Hakika hiyo haitakuwa kazi rahisi.

Lakini pia, papo kwa papo kamba hukata jiwe; iwapo Dkt Ruto ataendelea kuzuru maeneo yanayosawiriwa kama ngome ya Raila kisha ahakikishe nayo pia yanapata maendeleo, kwa kiwango fulani atafifisha hisia za chuki za kikabila zilizoibuliwa na cheche za matusi katika uchaguzi mkuu uliopita.

Rais atatembelea kaunti za Nyanza kuanzia leo ambako anatarajiwa kuzindua miradi ya maendeleo. Hiyo ni hatua nzuri inayofaa iungwe mkono na kila mtu mwenye nia njema.

Hata hivyo, muhimu zaidi ni Dkt Ruto kuhakikisha hapana wakati mwingine tena, hasa uchaguzini, ambapo wanasiasa wataruhusiwa kuibua mihemko na hisia za chuki za kikabila miongoni mwa wananchi.

  • Tags

You can share this post!

Viungo vya kujitengenezea vinavyodhuru ngozi yako baada ya...

Kipa Hugo Lloris wa Ufaransa astaafu soka ya kimataifa

T L