• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Kipa mdogo kiumri mwenye uzoefu langoni

Kipa mdogo kiumri mwenye uzoefu langoni

NA PATRICK KILAVUKA

KOMEO Maxwell Odhiambo, 17, mwanafunzi wa Kidato cha Nne Sekondari ya Jamhuri High, Kaunti ya Nairobi ni mwiba langoni.

Amejishindia matuzo manne akichezea timu za mtaani. Mbali na kuwa mchumani mwa timu ya shule anakosomea inayojulikana kama Pelico Jam ambayo inayocheza Ligi ya Kaunti, FKF, Nairobi West.

Isitoshe, anadakia pia timu ya Nairobi Water ambayo inashiriki Ligi ya Daraja la Pili, licha ya umri wake.

Mdakaji Odhiambo alisomea Shule ya Msingi ya Kaloleni, Kaunti ya Nairobi kabla kujiunga na Shule ya Upili ya Kakamega baada ya talanta yake kuwa kivutio cha kupata ufadhili wa masomo shuleni humo.

Moja kwa moja alisajiliwa katika timu ya shule hiyo almaarufu kama Green Commandos na kuicheza kwa miaka miwili akiwa kidato cha kwanza na pili ambapo aliiwezesha kufika kiwango cha kitaifa katika michezo za shule za upili.

Isitoshe, ndoto yake ya jaha ambayo inamuandama tangia akiwa shule ya msingi alikoanzia soka akiwa Darasa la Nne, iliendelea kumng’aria hadi akakwea hadi mashindano ya kiwango cha kitaifa.

Hata hivyo, jicho pevu la kocha Fredrick Amollo aliye mkufunzi wa soka wa Shule ya Upili ya Jamhuri High, lilimtazama. Alifua dafu tena kurudi jijini Nairobi baada ya kusajiliwa na shule hiyo.

“Wakati wa mashindano ya shule za upili, niliuona uwezo wake langoni na kumnyemelea kuimarisha nguzo ya mlinda langoni kikosini na sasa amekuwa moto wa kuotea mbali,” anasema kocha huyo ambaye amemwaminia nafasi hiyo kama kipa wa kwanza.

Ameihudumu timu hii ya shule kwa miaka miwili mtawalia akiwa kidato cha tatu na cha nne ikiwa inashiriki katika Ligi ya Kaunti, FKF, Nairobi West.

Mwaka 2021 aliiwezesha Pelico Jam kushikilia nafasi ya tatu katika jedwali la ligi hiyo na mwaka huu, anayomatumaini ya kudumisha uhai langoni na kuiwezesha imalize katika nafasi bora tatu.

Kipa Fredrick Odhiambo akiongoza kikosi cha Pelico Jam kupasha misuli kabla ya mechi dhidi ya FC Talents uwanjani, Kihumbuni. PICHA | PATRICK KILAVUKA

Matuzo ambayo ameyaweka kabatini ni lile la kipa bora akichezea MASA, S Base akichezea Prosoccer, la wasiozidi miaka 11 akiwa kiotani mwa Syokimau Academy na lile la kipute cha King Kaka.

Mnyakaji Odhiambo anasema anawaenzi makipa kama nduguye Fredrick Odhiambo wa Sofapaka FC kutokana na mbinu yake ya mawasiliano na wachezaji ugani kudhibiti ngome yake ya ulinzi na uokoaji wa mpira za krosi hatari ambazo zinasukumwa.

Kipa Fredrick Odhiambo akipanga safu ya ulinzi kudhibiti lango. PICHA | PATRICK KILAVUKA

Pia, mkamataji boli Alisson Becker wa Liverpool kutokana na njia rahisi ambazo anatumia kudhibiti lango na kuwa kipa mmakinifu.

Angependa majaliwa ya Jalali kuwa kipa wa kikosi cha Liverpool kutokana mchezo wa timu hiyo kulandana na udhibiti wake wa lango.

Anamwagia sifa kedekede nduguye Odhiambo ambaye anamtia hamasa na kumpiga jeki na vifaa vya kunyakia boli kama glava na buti.

Analo wazo kwa chikupizi kama yeye kwamba, wasife moyo safari ya kabumbu huenda hatua kwa hatua kwa kujituma, kujasirika na kuwa na maono ya kufikia ndoto zake kwani, boli ni taaluma.

  • Tags

You can share this post!

Akina mama wasababisha msongamano Nakuru wakisherehekea...

Historia yatia Karua doa kuhusu kupiga vita ufisadi...

T L