• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
Historia yatia Karua doa kuhusu kupiga vita ufisadi serikalini

Historia yatia Karua doa kuhusu kupiga vita ufisadi serikalini

NA TAIFA RIPOTA

MATUMAINI ya wengi kuwa Bi Martha Karua atasaidia kupigana na ufisadi na kuhakikisha utawala wa sheria umerudishwa nchini huenda yakawa ndoto.

Hii ni ikizingatiwa kuwa historia inaonyesha Bi Karua alipokuwa na fursa ya kukabiliana na ufisadi akiwa serikalini aliipoteza.

Mnamo 2006 akiwa Waziri wa Haki na Masuala ya Katiba, Bi Karua alipuuzilia mbali ripoti ya aliyekuwa mkuu wa Tume ya Kupambana na Ufisadi, John Githongo, ambayo iliwahusisha wanasiasa wakuu katika utawala wa Mwai Kibaki na kashfa ya Anglo Leasing.

Badala ya kuchukulikia ripoti ya Bw Githongo kwa uzito na kuifuatilia katika wadhifa wake kama waziri mhusika, Bi Karua aliitisha kikao cha wanahabari akiandamana na Raphael Tuju, ambaye alikuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni, ambapo walimkashifu Bw Githongo kama aliyekuwa akitumiwa na wafadhili kuharibia serikali sifa, na kuwa ripoti yake ilikuwa ni madai ya uwongo.

Baadaye kashfa hiyo ya Anglo Leasing ililipuka wazi ambapo ilibainika Kenya ilipoteza mabilioni ya pesa kupitia njama zilizohusisha baadhi ya mawaziri na wakuu serikalini.

Mnamo 2008, Bi Karua alitangaza kuwa aliyekuwa balozi wa Uingereza nchini, Edward Clay hangekubaliwa kukanyaga Kenya. Hii ni kufuatia kauli za Clay kuhusu uchaguzi wa 2007 uliokumbwa na ghasia ambapo alidai mrengo wa Kibaki ulikuwa umeiba kura.

Mwanadiplomasia huyo pia alikuwa mkosoaji mkubwa wa serikali kuhusu ufisadi ambao serikali ya Narc ilitarajiwa ingepigana nao ilipochaguliwa 2002.

Wakati mmoja aliitaja serikali hiyo kama iliyokuwa ikiongozwa na “walafi ambao baadaye walitapikia viatu vya wananchi”.

Mnamo 2013, Bi Karua alimkashifu Bw Raila Odinga akisema alifaa kustaafu pamoja na Kibaki kwa kile alichosema ni kushindwa kukabiliana na ufisadi ambao alidai ulikolea miongoni mwa wandani wake.

Alisema hakuwa na chochote alichokubaliana kuhusu na Bw Odinga.

Kubadilika kwa msimamo wake na kukubali kufanya kazi na mtu ambaye alimtaja kama aliyeshindwa kupigana na ufisadi kunazua tashwishwi zaidi kuhusu uwezo wa Bi Karua kuongoza vita dhidi ya ufisadi.

  • Tags

You can share this post!

Kipa mdogo kiumri mwenye uzoefu langoni

Uzalishaji wa mahindi, maharagwe na ngano washuka, bei...

T L