• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Kisasi tupu leo Real ikialika City

Kisasi tupu leo Real ikialika City

NA MASHIRIKA

MADRID, Uhispania

REAL Madrid watakuwa nyumbani ugani Santiago Bernabeu kukabiliana na Manchester City katika mechi ya marudiano ya nusu-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya baada ya kushindwa katika mkondo wa kwanza, wiki iliyopita.

Manchester City wanaingia uwanjani wakiwa na faida ya kushinda 4-3 kwenye mechi ya kwanza, lakini huenda juhudi zao zikavurugwa na mshambuliaji matata Karim Benzema ambaye kiwango chake kiko juu kwa sasa.

Bernardo Silva, Gabriel Jesus, Kevin De Bruyne na Phil Foden walifungia Manchester City, wakati Madrid wakipata yao kupitia kwa Benzema (2) na Vinicius Junior.

Wakilinda ushindi wao, watapata fursa ya kufuzu kwa fainali itakayochezewa Stade de France, Mei 28.

Misimu iliyopita Benzema hakuwahi kufunga mabao zaidi ya saba kwenye michuano hii lakini msimu huu amewasha moto.

Mshambuliaji huyo matata wa timu ya taifa ya Ufaransa anafukuza rekodi ya Cristiano Ronaldo ya kufunga mabao katika mashindano haya ndani ya msimu mmoja.

Kufikia sasa, anahitaji mabao matatu tu na kuvunja rekodi ya Ronaldo aliyefunga mabao 10 katika hatua ya mtoano.

Kocha Pep Guardiola anatarajiwa kuunda kikosi imara cha kumdhibiti nyota huyo mwenye umri wa miaka 34 ambaye kiwango chake kimeimarika zaidi chini ya kocha mkongwe Carlo Ancelotti.

Madrid waliibandua Paris Saint-Germain katika hatua ya 16-bora na Chelsea katika hatua ya robo-fainali, hata baada ya kushindwa nyumbani 3-2 na vigogo hao wa Ligi Kuu ya Uingereza.

Kabla ya mechi hiyo, Madrid walikuwa hawajashindwa na timu ya Uingereza ugani Santiago Bernabeu tangu Disemba 2018.

Wikendi waliibuka na ushindi mkubwa wa 4-0 dhidi ya Espanyol na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), wakati City wakiandikisha ushindi kama huo dhidi ya Leeds na kuendelea kuongoza msimami wa EPL, mbele ya Liverpool kwa tofauti ya pointi moja.

  • Tags

You can share this post!

Korti yaokoa mzazi kumpeleka mtoto katika shule ghali

DCI wachunguza kifo cha mwanawe mbunge maalum

T L