• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
Kitanuka Emirates leo!

Kitanuka Emirates leo!

NA MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

WENYEJI Arsenal na Manchester United zitavaana ugani Emirates katika mechi ya Ligi Kuu (EPL) iliyo na uwezo mkubwa wa kuweka hai ama kuzima kabisa ndoto zao za kushiriki Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Wanabunduki wa Arsenal wana motisha baada ya kunyamazisha Chelsea 4-2 uwanjani Stamford Bridge mnamo Aprili 20.

Pia, Arsenal hawajafungwa goli na United ligini katika michuano mitatu iliyopita uwanjani Emirates.

Walizoa ushindi wa 2-0 mnamo Machi 2019 na pia 2-0 mnamo Januari 2020, kabla kutoka 0-0 walipokutana mara ya mwisho katika uga huo Januari 2021.

Mbali na kutoshinda Gunners nyumbani kwao mara tatu mfululizo ligini, Red Devils wanauguza majeraha ya kucharazwa 4-0 na Liverpool siku ya Jumanne katika mechi za kati mwa wiki.

Vijana wa kocha Mikel Arteta, ambao walishiriki Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mara ya mwisho msimu 2016-2017, wanakamata nafasi ya tano kwa alama 57 baada ya kujibwaga uwanjani mara 32.

Wako nyuma ya nambari nne Tottenham Hotspurs ila kwa tofauti ya ubora wa magoli.

Kwa upande wao, masogora wa Ralf Rangnick wanapatikana nafasi ya sita na pointi 54 katika mechi 33.

Macho hapa yatakuwa kwa mastraika Eddie Nketiah na Cristiano Ronaldo.

Nketiah alichangia mabao mawili Arsenal ikizamisha Chelsea katikati mwa wiki.

Arsenal haijawahi kupoteza kinda huyo anapopata bao. Imeshinda mechi 15 na kutoka sare mara moja katika mechi ambazo mshambulizi huyo ameona lango.

Gunge Ronaldo alikosa mchuano wa Liverpool akiomboleza kifo cha mwanawe wa kiume mchanga, lakini alirejea mazoezi na huenda akaongoza mashambulizi ya United leo.

Viongozi Manchester City wataalika nambari 19 Watford wakitumai kuongeza mwanya dhidi ya Liverpool hadi alama nne.

Kikosi cha Pep Guardiola kinafukuzia ushindi wa 15 mfululizo dhidi ya Watford katika mashindano yote.

You can share this post!

Fujo za baada ya uchaguzi zilivyomharibia Kibaki sifa

Jimmy: Jaramogi alimsaidia sana Kibaki kuingia siasa

T L