• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
Kituo cha OlympAfrica cha kukuza talanta za michezo kuanza kujengwa Ruai miezi mitatu ijayo

Kituo cha OlympAfrica cha kukuza talanta za michezo kuanza kujengwa Ruai miezi mitatu ijayo

NA AYUMBA AYODI

UJENZI wa kituo cha kisasa cha kukuza talanta cha OlympAfrica katika uwanja wa Muhuri Muchiri mtaani Ruai katika kaunti ndogo ya Kasarani jijini Nairobi, utaanza miezi mitatu ijayo.

Kituo hicho ni matunda ya mkataba kati ya Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki Kenya (NOC-K), wakfu wa OlympAfrica na serikali ya Kaunti ya Nairobi.

Ndoto ya Kenya kuwa taifa la 38 barani Afrika kuwa na kituo cha chipukizi cha OlympAfrica ilianza kuchukua mwelekeo mzuri hapo Jumatano baada ya Kaunti ya Nairobi kupatia rasmi NOC-K shamba la ekari 10 ambalo ilikuwa imeahidi kwa ujenzi wa kituo hicho.

Kaimu Gavana wa Nairobi, Ann Kananu na rais wa NOC-K Paul Tergat, ambaye alikuwa ameandamana na meneja wa miradi ya OlympAfrica, Yaye Ndiate Sall walisaini mkataba ambao sasa umeidhinisha ujenzi wa kituo hicho uanze.

“Siku ya leo ni ya kihistoria kwa sababu inaipa Nairobi fursa ya kuwa na kituo cha kisasa cha michezo ambacho kitasaidia chipukizi wetu kukuza talanta zao,” alisema Kananu akidokeza kuwa mara kituo hicho kitakapokamilika, kitahudumia watoto kutoka mitaa ya Ruai, Mwiki, Mihango, Utawala, Kasarani, Kamulu na kutoka hata kaunti jirani za Kiambu na Machakos.

“Maeneo haya yana idadi kubwa ya vijana ambao, mbali na kutumia kituo hicho kukuza talanta zao, pia watapata kujiondoa ama kujitenga na visa vya maovu kama uhalifu, dawa za kulevya na uraibu wa pombe,” alisema Kananu ambaye aliandamana na maafisa kadhaa wa ngazi ya juu wa Kaunti ya Nairobi wakiwemo Janet Ouko (Waziri wa Elimu na Michezo) na Charles Kerich (Waziri wa Ardhi).

Kananu anatumai kuwa kituo hicho siku moja kitaweza kutoa mashujaa wa Olimpiki kama Paul Tergat, Paul Ereng, Robert Wangila, Pamela Jelimo na Nancy Lagat, miongoni mwa wengine.

Mbali na kutoa ardhi ya bure, Kananu alisema atahakikisha kuwa NOC-K itapata usaidizi wowote itahitaji kutoka kwa mshirika wao Nairobi Metropolitan Services (NMS), ambao watashughulikia kuimarisha barabara, maji, umeme na mahitaji mengine kwa kituo hicho. Aliongeza kuwa anatumai kuwa kaunti ndogo 16 zilizosalia zitapata kuwa na vifaa kama hivyo siku za usoni.

Ndiate alisema kuwa OlympAfrica itatoa Sh35 milioni (Dola za Amerika 350,000) kufanikisha awamu ya kwanza ya ujenzi ambao utaanza na uwanja wa soka na sehemu ya wanariadha kukimbilia kabla ya vifaa hivyo vingine.

Tergat alisema kuwa anatarajia ujenzi uanze miezi mitatu ijayo na kuongeza kuwa kituo hicho kitawapa watoto motisha ya kujiingiza katika michezo. Alifichua kuwa ataomba fedha zaidi kutoka kwa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) na Shirikisho la Kamati za Kitaifa za Olimpiki barani Afrika (Anoca) ili kufanya mradi huo ufaulu.

Kituo chenyewe kitakuwa na ukumbi unaoweza kutumika kwa michezo tofauti ikiwemo voliboli, mpira wa vikapu, handiboli, tenisi na bwawa la kuogelea.

Kitakuwa pia na mabweni, kituo cha afya, eneo la mashabiki kukaa pamoja na mgahawa.

Wakfu wa OlympAfrica ulianzishwa miaka 25 na marais wa zamani wa IOC ili kutoa fursa kwa vijana kutoka Bara Afrika kukuza na kujiinua kimichezo.

TAFSRI: GEOFFREY ANENE

  • Tags

You can share this post!

Namcos afurahia World Rugby kutangaza kurejea kwa Raga za...

Fujo, hongo kwenye uchaguzi mdogo Nakuru