• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Namcos afurahia World Rugby kutangaza kurejea kwa Raga za Dunia

Namcos afurahia World Rugby kutangaza kurejea kwa Raga za Dunia

Na GEOFFREY ANENE

Kocha Innocent ‘Namcos’ Simiyu ameelezea furaha yake kuwa Shirikisho la Raga Duniani limetangaza kurejea kwa mashindano ya Raga za Dunia ya wachezaji saba kila upande kuanzia mwezi Mei 2021.

World Rugby imesema Jumatano kuwa mashindano hayo ya kifahari yataanza na duru mbili za kinadada jijini Paris nchini Ufaransa mnamo Mei 15-16 na Mei 22-23. Duru ya kwanza ya wanaume itakuwa ile ya Singapore Sevens mnamo Oktoba 29-30, ingawa inaweza kuwa mapema kwa sababu shirikisho hilo linazungumza na Canada na Uingereza kuona kama zinaweza kuandaa duru zao baada ya michezo ya Olimpiki itakayofanyika kati ya Julai 23 na Agosti 8 jijini Tokyo, Japan. Duru nyingine zitakuwa za mseto. Zitaleta mashindano ya kinadada na wanaume mjini Hong Kong (Novemba 5-7), Dubai (Desemba 3-4) na Cape Town (Desemba 10-12).

Akizungumza na Taifa Leo kuhusu tangazo hilo ambalo limepokekewa kwa furaha na wanaraga na wapenzi wa mchezo huo, Namcos amesema, “Tunafurahia kuwa hali ya kawaida inarejea.”

Kocha huyo wa timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya wanaume almaarufu Shujaa, aliwasili Jumatatu nyumbani na vijana wake kutoka Uhispania walikomaliza Madrid Sevens mara mbili katika nafasi ya pili.

“Tuko mapumzikoni sasa hadi Jumatatu ijayo tutakapoanza mazoezi tena kwa timu iliyokuwa Madrid. Wake walio kikosini, lakini hawakusafiri wanaendelea na mazoezi uwanjani KRU. Tutaingia kambi ya mazoezi ya Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki Kenya (NOC-K) juma lijalo,” alisema.

Kenya ni mojawapo ya mataifa yanayoshiriki duru zote za Raga za Dunia. Washiriki wengine wa raga hizo ni New Zealand, Afrika Kusini, Fiji, Amerika, Australia, Uingereza, Scotland, Wales, Ufaransa, Samoa, Uhispania, Ireland, Canada na Japan.

Mabingwa wa Afrika Kenya walikamilisha msimu wa 2019-2020 uliovurugwa na mkurupuko wa virusi vya corona katika nafasi ya 12 kwa alama 35 walizovuna kutoka Dubai (nne), Cape Town (11), Hamilton (10), Sydney (moja), Los Angeles (tatu) na Vancouver (sita). Duru za Hong Kong, Singapore, Ufaransa na London zilifutiliwa mbali kutokana na janga hilo. Raga za Dunia hazijachezwa tangu baada ya duru za Los Angeles na Vancouver mwezi Machi 2020.

  • Tags

You can share this post!

Rangers ya kocha Steven Gerrard sasa watia mkono mmoja...

Kituo cha OlympAfrica cha kukuza talanta za michezo kuanza...