• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Kocha Erik Ten Hag wa Ajax kupokezwa na Man-United mkataba wa miaka mitatu

Kocha Erik Ten Hag wa Ajax kupokezwa na Man-United mkataba wa miaka mitatu

Na MASHIRIKA

KOCHA Erik ten Hag wa Ajax nchini Uholanzi ataanza kunoa kikosi cha Manchester United kwa mkataba wa miaka mitatu mwishoni mwa msimu huu.

Mkufunzi huyo raia wa Uholanzi mwenye umri wa miaka 52 atakuwa radhi kurefusha kanadarasi yake uwanjani Old Trafford kwa mwaka mmoja zaidi kutegemea matokeo yake kambini mwa Man-United.

Atajaza nafasi ya kocha mshikilizi Ralf Rangnick aliyeaminiwa fursa ya kushikilia mikoba ya Man-United mnamo Novemba 2021 baada ya mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kuagana na kocha raia wa Norway, Ole Gunnar Solskjaer.

Kocha wa zamani wa Tottenham Hotspur ambaye sasa anadhibiti mikoba ya Paris St-Germain (PSG) ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1), Mauricio Pochettino alikuwa pia akipigiwa upatu wa kupokezwa mikoba ya Man-United.

Ten Hag atapokezwa mkataba wa Man-United kirasmi wakati wowote baada ya kuongoza Ajax kumenyana na PSV Eindhoven kwenye fainali ya Dutch Cup mnamo Aprili 17, 2022.

Kufikia sasa, Ajax wanadhibiti kilele cha Ligi Kuu ya Uholanzi (Eredivisie) kwa alama nne zaidi kuliko nambari mbili PSV ambao wamejizolea alama 68 kutokana na mechi 29 zilizopita.

Ajax walidenguliwa na Benfica ya Ureno katika hatua ya 16-bora kwenye kampeni za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu wa 2021-22. Rekodi ya kushinda mechi moja pekee kutokana na saba zilizopita katika mashindano yote ndiyo duni zaidi kuwahi kushuhudiwa kambini mwa Man-United tangu 2019.

Matumaini ya kikosi hicho kukamilisha kampeni za EPL msimu huu ndani ya orodha ya nne-bora na hatimaye kufuzu kwa soka ya UEFA msimu ujao wa 2022-23 pia ni finyu sana. Kwa sasa wanakamata nafasi ya saba jedwalini kwa alama 51, sita nyuma ya Tottenham wanaofunga mduara wa nne-bora.

Kibarua kigumu zaidi kwa Ten Hag ni kushughulikia mustakabali wa kitaaluma wa wanasoka Paul Pogba, Jesse Lingard, Cristiano Ronaldo na Marcus Rashford wanaohusishwa na uwezekano mkubwa wa kuondoka Old Trafford mwishoni mwa muhula huu.

Ten Hag atakuwa kocha wa tano baada ya David Moyes, Louis van Gaal, Jose Mourinho na Solskjaer kupokezwa wa mkataba wa kudumu kambini mwa Man-United tangu mkufunzi Sir Alex Ferguson astaafu mnamo 2013.

You can share this post!

Aliyekuwa kapteni wa Colombia, Freddy Rincon, aaga dunia...

Sokomoko bungeni Gedi akieleza madai ya jinsi Ruto hunyakua...

T L