• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Kocha Joachim Loew arejesha wanasoka Muller na Hummels katika timu ya taifa ya Ujerumani

Kocha Joachim Loew arejesha wanasoka Muller na Hummels katika timu ya taifa ya Ujerumani

Na MASHIRIKA

FOWADI wa Bayern Munich, Thomas Muller na beki matata wa Borussia Dortmund, Mats Hummels wamerejeshwa katika timu ya taifa ya Ujerumani na sasa watakuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa kwenye fainali zijazo za Euro.

Kocha Joachim Loew amejumuisha wawili hao kwenye kikosi chake licha ya kuwaambia mnamo Machi 2019 kwamba hawakuwa kabisa katika mawazo wala mipango yake ndani ya timu ya taifa.

Muller, 31, amefungia Bayern jumla ya mabao 11 na kuchangia mengine 18 katika kampeni za Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) msimu huu. Mchango wake huo ni kiini cha miamba hao kuhifadhi ufalme wa taji hilo chini ya kocha Hansi Flick atakayeagana nao rasmi mwishoni mwa msimu huu.

Kwa upande wake, Hummels mwenye umri wa miaka 32, alisaidia waajiri wake Dortmund kukomoa RB Leipzig na kutia kibindoni taji la German Cup muhula huu.

Kupitia akaunti zao za Instagram, Muller alisema, “Nimerejea tena” huku Hummels akiandika, “Nina furaha ya kurudi kikosini” na niko tayari kwa ukurasa mpya kitaaluma”.

Chini ya kocha Loew ambaye atajiuzulu mwishoni mwa fainali za Euro mwaka huu, Ujerumani walipigwa 6-0 na Uhispania kwenye kipute cha UEFA Nations League mnamo Novemba 2020.

Hicho ndicho kichapo kinono zaidi kwa mabingwa hao mara nne wa Kombe la Dunia kuwahi kupokea katika historia ya mashindano yoyote. Nafasi ya Loew kambini mwa Ujerumani inatarajiwa kutwaliwa na kocha Flick.

“Unaweza ukavuruga mpangilio wa kikosi wakati fulani haja inapolazimu. Timu imekuwa ikusuasua kwenye safu ya ulinzi. Mats ataleta mwamko mpya na atazidisha viwango vya ushindani katika idara hiyo,” akasema Loew.

Chipukizi Jamal Musiala, 18, amejumuishwa pia na kocha Loew kwenye kikosi chake. Kinda huyo aliyekuwa katika akademia ya Chelsea kabla ya kutua Bayern mnamo 2019, aliteua kuwakilisha Ujerumani badala ya Uingereza au Nigeria kwenye soka ya kimataifa.

Ujerumani wametiwa kwenye Kundi F kwa pamoja na Ufaransa, Hungaru na mabingwa watetezi Ureno katika mashindano ya Euro yatakayoanza Juni 11 hadi Julai 11 baada ya kuahirishwa mnamo 2020 kwa sababu ya corona. Loew ataongoza kikosi chake kufungua rasmi kampeni za kipute hicho dhidi ya Ufaransa mnamo Juni 15, 2021.

KIKOSI CHA UJERUMANI:

MAKIPA: Manuel Neuer, Kevin Trapp, Bernd Leno.

MABEKI: Antonio Rudiger, Mats Hummels, Matthias Ginter, Niklas Suele, Emre Can, Lukas Klostermann, Robin Gosens, Robin Koch, Christian Gunter, Marcel Halstenberg.

KIUNGO: Joshua Kimmich, Ilkay Gundogan, Kai Havertz, Toni Kroos, Leon Goretzka, Leroy Sane, Jonas Hofmann, Florian Neuhaus, Jamal Musiala.

WAVAMIZI: Serge Gnabry, Thomas Muller, Timo Werner, Kevin Volland.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Ni rasmi kuwa Martha Koome ndiye Jaji Mkuu wa Kenya

Kenya yakabiliwa na uhaba mkubwa wa chanjo ya corona