• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
Kocha McCrath kutegemea ujuzi wake kuvumisha Kenya Sevens

Kocha McCrath kutegemea ujuzi wake kuvumisha Kenya Sevens

AYUMBA AYODI na JOHN ASHIHUNDU

KOCHA mpya wa timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande (Kenya Sevens), Damian McGrath anatarajia uzoefu wake kumsaidia kutimiza malengo yake ya muda mfupi ya kuiwezesha Kenya kuvuma.

Mwingereza huyo mwenye umri wa miaka 64 amesema Kenya itapiga hatua kama zilivyopiga timu za mataifa ya Samoa, Uingereza, Canada na Ujerumani.

“Nimekuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Uingereza kwa miaka mingi na kufalulu katika utenda kazi wangu ukiwemo ushindi dhidi ya timu ya Hong Kong. Nilikuwa kocha mkuu wa timu ya Samoa, Canada na Ujerumani ambazo zilifaulu katika mashindano mbali mbali,” McGrath alisema jana baada ya kujulishwa rasmi kama kocha wa timu ya Kenya Sevens.

McGrath, anayechukuwa mikoba kutoka kwa Innocent “Namcos” Simiyu alisema kilichomfanya akubali kazi hiyo ni umaarufu wa kikosi cha Kenya katika mashindano ya kimataifa.

“Timu ya Kenya ina wachezaji wa vipaji vya hali ya juu na ilipopata nafasi hii niliitwaa kwa mikono yote miwili,” McGrath alieleza, huku akiongeza kwamba aliweza kuwashuhudia alipokuwa hapa nchini na timu ya taifa ya Ujerumani mwaka uliopita.

“Kupata fursa ya kunoa timu ya kiwango hiki ni jambo la kujivunia. Muhimu ni kujitahidi mazoezini ndipo tufaulu katika malengo yetu,” alisema McGrath.

“Jamii yangu na marafiki wamefurahia kwamba nimepata nafasi hii kubwa,” aliongeza McGrath, anayejinia ujuzi wa miaka 30 kama kocha.

Mtihani wa kwanza wa McGrath na mashindano ya Toulouse Sevens yatakayofanyika Mei 20-22 ugani Stade Ernest-Wallon, Ufaransa, kabla ya London Sevens zitakazofanyika Mei 28-29 kule Twickenham Stadium, nchini Uingereza.

Archadius Khwesa na Ben Salem huenda wakajipata kikosini kwa mara ya kwanza wakati wa mashindano hayo ya Toulouse na London ambayo ni mchujo wa mechi za Kombe la Dunia za msimu wa 2021/2022 (World Rugby Sevens).

Wawili hao pamoja na Alvin Otieno, Timothy Mmasi na Johnstone Olindi ndio wageni pekee kwenye kikosi kilichoshiriki michuano ya mchujo ya Singapore na Vancouver Sevens.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Ruto atueleze jinsi atakavyozima ufisadi...

Malalamiko ya wabunge baada ya SRC kupunguza mapato yao

T L