• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 3:13 PM
Kocha Nigel Pearson apata kazi kambini mwa Bristol City

Kocha Nigel Pearson apata kazi kambini mwa Bristol City

Na MASHIRIKA

BRISTOL City wamempa Nigel Pearson, 57, mikoba yao ya ukufunzi hadi mwishoni mwa muhula huu.

Mkufunzi huyo wa zamani wa Leicester City na Watford hajakuwa na klabu tangu aagane na Watford zikisalia mechi mbili kabla ya kampeni za msimu uliopita wa 2019-20 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kutamatika.

Kuajiriwa kwake kulichochewa na haja ya kujaza pengo la Dean Holden aliyefutwa kazi kwa sababu ya matokeo duni ya kikosi cha Bristol.

Pearson aliyeanza kazi ya ukufunzi kambini mwa Carlisle, amewahi pia kudhibiti mikoba ya Southampton, Hull City na Derby County.

Kufikia sasa, Bristol almaarufu The Robins, wanashikilia nafasi ya 15 kwenye msimamo wa jedwali la Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Uingereza (Championship) na wana alama 10 zaidi nje ya mduara wa kushuka ngazi licha ya kupoteza msururu wa mechi saba zilizopita.

Rekodi hiyo duni ilichangia kupigwa kalamu kwa Holden mnamo Februari 17 japo wakapigwa tena na Barnsley katika mchuano wao uliopita chini ya kocha mshikilizi Paul Simpson.

Pearson anatarajiwa kuanza kazi haraka iwezekanavyo na kibarua chake cha kwanza kambini mwa Bristol ni mechi ya ligi itakayowakutanisha na Middlebrough mnamo Februari 23 kabla ya kuwaendea Swansea City mnamo Februari 27, 2021.

Pearson aliwahi kuwaongoza Leicester kuingia katika mashindano ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2014 baada ya kuwatoa ndani ya mduara wa vikosi vitatu vya mwisho baada ya kushinda mechi saba na kuambulia sare mara moja kutokana na mechi 10 za mwisho msimu huo.

Aliondoka mwishoni mwa msimu wa 2014-15 na kikosi alichokisuka uwanjani King Power ndicho kilichotegemewa na kocha Claudio Ranieri kuwavunia Leicester ufalme wa EPL mnamo 2015-16.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Mswada wa BBI wakaribia kuingia katika Bunge la Kitaifa

Masoud Juma, Duncao Ochieng’ wachana nyavu katika...