• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Kocha Vieira kurejea Arsenal kuwinda vipaji vya kuboresha Crystal Palace

Kocha Vieira kurejea Arsenal kuwinda vipaji vya kuboresha Crystal Palace

Na MASHIRIKA

KOCHA Patrick Vieira wa Crystal Palace amefichua mipango ya kurejea katika vikosi vyake vya zamani – Arsenal na Nice – ili kujinasia huduma za wanasoka Eddie Nketiah na Kasper Dolberg mtawalia.

Vieira anayelenga kuisuka upya klabu ya Palace, amesisitiza kwamba waajiri wake wako radhi kuweka mezani kima cha Sh3.1 bilioni kwa ajili ya Nketiah.

Nketiah, 22, atakuwa radhi kuondoka uwanjani Emirates baada ya majaribio yake ya miaka mingi kupata uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza kugonga mwamba.

Palace wanahemea pia maarifa ya Dolberg na wako tayari kuweka mezani Sh3.9 bilioni kwa ajili ya fowadi huyo wa Denmark. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 23 alisajiliwa na Vieira kutoka Ajax misimu miwili iliyopita akidhibiti mikoba ya Nice ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).

Dolberg aliibuka mfungaji bora wa Nice katika msimu wake wa kwanza kwenye Ligue 1. Makali yake yalishuka pakubwa katika msimu wa pili ulioshuhudia Vieira akipigwa kalamu mnamo Disemba 2020. Hata hivyo, ufufuo wa makali yake ulidhihirika majuzi alipoongoza Denmark kutinga nusu-fainali za Euro.

Mbali na kuwania huduma za Nketiah na Dolberg, Palace wanavizia pia wanasoka Ismaila Sarr, 23, na Victor Nelsson, 22. Wawili hao wanachezea Watford na Copenhagen FC mtawalia.

Chini ya kocha Mikel Arteta, Arsenal tayari wamesajili kiungo Albert Sambi Lokonga kutoka Anderlecht ya Ubelgiji pamoja na beki Nuno Tavares wa Benfica inayoshiriki Ligi Kuu ya Ureno.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Mkenya aliyechapwa viboko na Mchina kulipwa Sh3 milioni

JAMVI: Uhuru, Ruto mbioni kudhihirisha ubabe Mlima Kenya