• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
JAMVI: Uhuru, Ruto mbioni kudhihirisha ubabe Mlima Kenya

JAMVI: Uhuru, Ruto mbioni kudhihirisha ubabe Mlima Kenya

Na WANDERI KAMAU

UCHAGUZI mdogo wa eneobunge la Kiambaa, Kaunti ya Kiambu, unatarajiwa kutoa taswira kamili ya mpenyo wa kisiasa wa Naibu Rais William Ruto katika ukanda wa Mlima Kenya ielekeapo 2022.

Uchaguzi huo umepangiwa kufanyika Alhamisi ijayo, huku ukifasiriwa kama ushindani mkali wa kisiasa kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto.

Kulingana na wadadisi wa siasa, uchaguzi pia utakuwa jukwaa maalum kuonyesha ikiwa uungwaji mkono wa Rais Kenyatta umepungua Mlima Kenya, kama ambavyo imekuwa ikionekana na wengi.

Ingawa Rais Kenyatta hajakuwa akionekana kuwa na usemi wowote kwenye uchaguzi huo, hilo lilidhihirika wazi Alhamisi, wakati alikutana na kundi la viongozi wa Jubilee ambao wamekuwa wakikifanyia chama kampeni katika eneobunge hilo.

Ujumbe huo uliwashirikisha mwaniaji wa Jubilee katika eneobunge hilo, Bw Kariri Njama, wabunge Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini), Sabina Chege (Murang’a), Kanini Keega (Kieni) kati ya wengine.

Baada ya kikao hicho kilichofanyika katika Ikulu ya Nairobi, Bw Wambugu alisema kuwa Bw Njama tayari amepata “baraka za Rais Kenyatta.”“Rais aliahidi kusimama nasi hadi mwisho. Hakuna chochote kitakachotutisha,” akasema Bw Wambugu.

Bi Wanjiru alisema “wenyeji wa Kiambaa wana uamuzi wa kuendelea kuwa serikalini au kuingia katika Upinzani.”

Mpinzani mkuu wa Jubilee kwenye uchaguzi huo ni Bw John Njuguna Wanjiku maarufu kama “Ka Wanjiku” anayewania kwa tiketi ya chama cha UDA, kinachohusishwa na Dkt Ruto.

Kufuatia kikao hicho, wadadisi wanasema ni wazi Rais Kenyatta anafuatilia kwa kina na makini mwelekeo wa siasa za Mlima Kenya na anaimarisha upya ushawishi wake wa kisiasa, japo kwa umbali.

Kwa miaka mitatu kufikia sasa, kumekuwa na hofu katika ukanda huo kwamba Rais amekuwa akipoteza umaarufu wake, hasa baada ya kubuni handisheki na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Suala jingine ambalo limekuwa likionekana kutokumbatiwa na wenyeji ni mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI), wengi wakiutaja kutokuwa muhimu kutokana na changamoto za kiuchumi zinazoikabili nchi.

Hata hivyo, wadadisi wanasema ni wazi sasa Rais anafuatilia kwa kina siasa za ngome yake, ikizingatiwa anatarajiwa na wengi kuwa na usemi kwenye mchakato wa urithi wake 2022.

“Rais Kenyatta ni mwanasiasa mjanja, anayecheza kadi zake kikamilifu kwa kuwatumia washirika wake. Inaonekana kuwa matokeo ya uchaguzi mdogo wa eneobunge la Juja ulimwamsha kisiasa. Kinyume ilivyo Kiambaa, hakuonekana akihusika sana kwenye uchaguzi wa Juja. Ni taswira inayoachilia wazi kuwa kama mwanasiasa, anafuatilia yale yote yanayoendelea,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Kulingana na wadadisi, “mzinduko” wa Rais Kenyatta umechochewa pakubwa na tishio la kuongezeka kwa uasi unaomkabili katika ngome yake, hasa miongoni mwa viongozi wanaoegemea mrengo wa ‘Tangatanga’, ambao humuunga mkono Dkt Ruto.

Hilo pia linatajwa kuchangiwa na hatua ya baadhi ya wanasiasa katika ukanda huo kugura mrengo wa ‘Kieleweke’ na kujiunga na ‘Tangatanga.’

Wiki mbili zilizopita wabunge Gathoni wa Mucomba (Kiambu), Kago wa Lydia (Githunguri), David Gikaria (Nakuru Mashariki) na Samuel Gachobe (Subukia) walihama ‘Kieleweke’ na kujiunga na ‘Tangatanga’, wakitaja maamuzi yao kuchangiwa na “uhalisia wa kisiasa ulio katika ukanda huo.”

“Huu si uamuzi wangu binafsi. Umechochewa na hali ilivyo kisiasa. Nimewasikiliza kwa kina wafuasi wangu, ambapo wengi wanaunga mkono mrengo wa ‘Hustler Nation’ wake Dkt Ruto. Nimechukua uamuzi huu baada ya kutathmini hali ilivyo kwa zaidi ya miezi miwili,” akasema Bi Wamuchomba.

Wadadisi wa siasa wanaeleza sababu nyingine inayomfanya Rais Kenyatta kufanya kila awezalo kuhakikisha Jubilee imetwaa ushindi katika eneo hilo ni kuhofia “kushindwa nyumbani kwake kwa mara ya pili.”

“Kiambaa imo katika Kaunti ya Kiambu, anakotoka Rais. Itakuwa pigo kubwa kisiasa ikiwa atashindwa kwa mara hii, kwani itaonekana ameshindwa kudhibiti ngome yake kabisa. Itakuwa taswira mbaya na itakayokuwa na athari kubwa kisiasa kwake,” asema Prof Ngugi Njoroge, ambaye ni mdadisi wa siasa za Kati.

Kulingana naye, matokeo hayo pia yataamua mwelekeo wa kisiasa utakaofuata, hasa kwenye uhusiano uliodorora kati yake na Dkt Ruto.

“Ikiwa Jubilee itashindwa, basi hilo litaonekana kama mjeledi wa pili kwa serikali. Huenda tukaona juhudi zaidi kuwakabili viongozi wanaoegemea mrengo wa Tangatanga. Ikiwa Jubilee itaibuka mshindi, basi inamaanisha kuwa juhudi za Rais kuanza kurejea kudhibiti ngome yake zimeanza kuzaa matunda,” akasema Prof Njoroge.

Licha ya hayo, wanasiasa katika pande zote wanashikilia kuwa mrengo wao utaibuka mshindi kwani “ndio unawakilisha na kuangazia matakwa ya wananchi.”

“Tushamaliza kinyang’anyiro cha Kiambaa. Imani yetu ni kuwa wenyeji wataikataa serikali inayowanyanyasa na kuukumbatia mrengo wa ‘Hustler’ (Watu wa Kawaida) unaomtambua na kumpa kipaombele mwananchi,” akasema mbunge Ndindi Nyoro (Kiharu).

Jubilee imeapa kudhihirisha bado ipo ngangari kama ilivyokuwa 2013 na 2017.

You can share this post!

Kocha Vieira kurejea Arsenal kuwinda vipaji vya kuboresha...

JAMVI: Kalonzo alivyowazidimaarifa magavana wa Ukambani