• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 9:50 AM
Lampard, Terry na Vieira wapigania nafasi ya kuwa kocha wa Bournemouth

Lampard, Terry na Vieira wapigania nafasi ya kuwa kocha wa Bournemouth

Na MASHIRIKA

ALIYEKUWA mwanasoka matata wa Arsenal, Patrick Vieira amejiunga na wachezaji wa zamani wa Chelsea – John Terry na Frank Lampard kuwania nafasi ya kuwa kocha wa Bournemouth waliotemwa kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mwishoni mwa msimu wa 2019-20.

Nafasi ya kocha mkuu kambini mwa Bournemouth ilisalia wazi mnamo Februari 3, 2021 baada ya kikosi hicho ambacho kwa sasa kinashiriki Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Uingereza (Championship) kumtimua mkufunzi Jason Tindall baada ya miezi sita pekee.

Kufikia sasa, Bournemouth almaarufu The Cherries wanashikilia nafasi ya sita kwenye msimamo wa jedwali la Championship baada ya kupoteza jumla ya michuano minne iliyopita kwa mfululizo.

Vieira kwa sasa hana kazi tangu apokonywe mikoba ya Nice kutokana na matokeo duni kwenye Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mnamo Disemba 2020. Kiungo huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa alipigwa kalamu na Nice baada ya kuhudumu katika Ligue 1 kwa kipindi cha miaka miwili na nusu pekee.

Akiwa Nice, Vieira, 44, aliowaongoza waajiri wake hao kutinga nafasi ya saba kwenye msimamo wa jedwali la Ligue 1 katika msimu wa kwanza kabla ya kuwapaisha hadi nafasi ya tano kwenye msimu wake wa pili.

Hata hivyo, msururu wa matokeo duni yaliyoshuhudia Nice ikipoteza mechi tano mfululizo kabla ya Krismamsi ya 2020 ulichochea usimamizi kumtema Vieira ambaye pia anahusishwa na mikoba ya Sheffield United ambao kwa sasa wanavuta mkia wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Kabla ya kutua Nice, Vieira alikuwa pia amedhibiti mikoba ya New York City inayoshiriki Major League Soccer (MLS) nchini Amerika kwa kipindi cha miaka miwili.

Lampard anaanza kuhusishwa na uwezekano wa kutwaa mikoba ya Bournemouth siku chache baada ya kufutwa kazi na Chelsea.

Kwa upande wake, Terry kwa sasa ni kocha msaidizi wa Aston Villa wanaonolewa na mkufunzi Dean Smith kwenye kampeni za EPL.

Mbali na watatu hao, kocha mwingine anayehusishwa na mikoba ya Bournemouth ni beki wa zamani wa Real Madrid na timu ya taifa ya Uingereza, Jonathan Woodgate ambaye kwa sasa anashikilia mikoba ya kikosi hicho tangu Tindall apigwe kalamu.

Mchuano ujao wa Bournemouth ni kibarua kikali kitakachowakutanisha na Birmingham City ugenini mnamo Februari 6, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Real kumwajiri Allegri iwapo Zidane ataondoka

Kivumbi kati ya Rotich na Kinyamal mbio za Relays zikiingia...