• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Kivumbi kati ya Rotich na Kinyamal mbio za Relays zikiingia mkondo wa lala salama

Kivumbi kati ya Rotich na Kinyamal mbio za Relays zikiingia mkondo wa lala salama

Na AYUMBA AYODI

Kivumbi kinatarajiwa wakati wanariadha nyota Ferguson Rotich na Wycliffe Kinyamal watakutana katika mchujo wa duru ya mwisho ya mbio za kupokezana vijiti uwanjani Nyayo hapo Jumamosi.

Rotich ni mshindi wa medali ya shaba ya Riadha za Duniani wa mita 800 naye Kinyamal ni bingwa wa Jumuiya ya Madola wa mbio hizo za mizunguko miwili.

Duru hiyo ya tatu itapisha mashindano ya kitaifa ya kuchagua timu ya Kenya itakayoshiriki Riadha za Dunia za kupokezana vijiti yatakayofanyika uwanjani humo mnamo Machi 26-27. Riadha za Dunia za kupokezana vijiti zitaandaliwa mjini Silesia, Poland mnamo Mei 1-2.

Katika duru ya tatu na mwisho ya kitaifa ya Shirikisho la Riadha Kenya (AK), Rotich na Kinyamal wametiwa katika kundi moja ambalo pia liko na mshindi wa medali ya fedha ya mbio za mita 800 ya Riadha za Afrika za chipukizi mwaka 2011 Jeremiah Mutai na bingwa wa Riadha za Dunia za makinda mwaka 2016 Kumari Taki.

Kwenye duru iliyopita (Januari 23), Mutai, ambaye alikuwa katika timu ya Kenya ya mita 4×800 kwenye Riadha za Dunia za kupokezana vijiti mwaka 2015 na Riadha za Dunia 2013 na Riadha za Dunia za Ukumbini 2014, aliandikisha kasi ya juu akishinda kundi lake kwa dakika 1:47.40.

Kinyamal aling’ara katika kundi la pili kwa dakika 1:47.77, Cornelius Tuwei akaandikisha kasi ya tatu bora (1:47.80) akifuatiwa na Taki (1:48.03). Rotich alishiriki mbio za mita 400.

Vita vikali pia vinatarajiwa katika katika kitengo cha kinadada cha mita 800 ambapo bingwa wa Kenya wa mbio za mita 400 Mary Moraa atamenyana na mshindi wa Kombe la Continental 2018 Winny Chebet katika kundi la kwanza. Emily Cherotich na Josephine Chelangat wako katika kundi la pili.

Moraa alitimka kasi ya juu katika mbio za mita 800 kwa dakika 2:04.92 katika duru iliyopita.

Kivumbi kilichotarajiwa katika mbio za mita 100 kati ya mshikilizi wa rekodi ya Kenya Mark Otieno na Ferdinand Omanyala, hakitakuwepo.

Omanyala, ambaye alitimka umbali huo kwa sekunde 10.11 akisaidiwa na upepo, pamoja na Boniface Mweresa, ambaye alishiriki mbio za mita 200, wamefungiwa nje kwa sababu waliwahi kukiuka sheria za kushindana bila kutumia dawa za kusisimua misuli. Wawili hawa wamekamilisha marufuku yao ya chini ya miaka miwili.

Mwanzoni, Naibu Rais wa AK Paul Mutwii alikuwa amesema kuwa wanariadha waliomaliza marufuku zao wanaweza kushiriki mashindano ya humu nchini, lakini si wakati timu ya taifa inachaguliwa.

Hata hivyo, kikao cha kamati kuu cha AK kiliamua hapo Februari 3 kuwapiga marufuku kabisa, ingawa wanaweza kujaribu bahati yao nje ya Kenya.

Otieno, ambaye anajivunia rekodi ya kitaifa ya mbio za mita 10.14, aliandikisha kasi ya pili ya juu katika duru iliyopita 10.32. Yuko katika kundi la pili ambalo linajumuisha Pius Muia (10.98) na Mathew Elijah (10.85). Mbio za mita 100 zitakuwa na makundi manne.

“Lengo langu kubwa ni kushiriki Olimpiki mjini Tokyo ambako natafuta medali bora kuliko ile ya shaba niliyopata kwenye Riadha za Dunia jijini Doha, Qatar mwaka 2019,” alisema Rotich, 31.

Kinyamal alisema amekuwa akisumbuliwa na majeraha tangu atawale mbio za mita 800 kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola 2018, “lakini niko fiti sasa”.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

You can share this post!

Lampard, Terry na Vieira wapigania nafasi ya kuwa kocha wa...

Kipa wa Ajax apigwa marufuku ya mwaka mmoja kwa kutumia...