• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Real kumwajiri Allegri iwapo Zidane ataondoka

Real kumwajiri Allegri iwapo Zidane ataondoka

Na MASHIRIKA

REAL Madrid watakuwa radhi kumpokeza kocha Massimiliamo Allegri au aliyekuwa jagina wao Raul Gonzalez mikoba ya ukufunzi iwapo watamtimua Zinedine Zidane mwishoni mwa msimu huu.

Zidane, 48, yuko katika presha ya kusajili matokeo bora uwanjani Santiago Bernabeu ikizingatiwa kwamba masogora wake wamekuwa wakisuasua katika kampeni za hadi kufikia sasa msimu huu.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) wanashikilia nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 40 sawa na Barcelona ya kocha Ronald Koeman.

Ingawa hivyo, ni pengo la alama 10 ndilo linalowatenganisha Real na viongozi wa jedwali, Atletico Madrid wanaonolewa na kocha Ronald Koeman.

Nafuu zaidi kwa Atletico ni kwamba wana mchuano mmoja zaidi wa kutandaza ili kufikia idadi ya mechi ambazo zimepigwa na washindani wao wakuu wakiwemo Barcelona, Real na Sevilla wanaofunga mduara wa nne-bora.

Kubwa zaidi lililochangia presha ya Zidane ambaye ni raia wa Ufaransa kambini mwa Real ni hatua ya waajiri wake kubanduliwa mapema na Alcoyano kwenye raundi ya tatu ya kivumbi cha Copa del Rey msimu huu.

Kwa mujibu wa gazeti la Cadena Ser Football Italia, Real almaarufu Los Blancos, wanawazia kumtimua Zidane mwishoni mwa msimu huu na kumpa mikoba ama Allegri au Raul.

Allegri hajawahi kupata kikosi cha kunoa tangu atimuliwe na miamba wa soka ya Italia, Juventus mnamo 2019 licha ya kuongoza kikosi hicho kutwaa mataji matano mfululizo ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Tangu afurushwe na Juventus, Allegri ambaye ni raia wa Italia amekuwa akihusishwa na vikosi vingi vya Ligi Kuu ya Uingereza vikiwemo Chelsea, Arsenal na Manchester United.

Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo, Bodi ya Usimamizi kambini mwa Real iko radhi kumwajiri Allegri kuliko Raul ambaye hana tajriba pevu wala uzoefu wa kutosha katika ulingo wa ukufunzi. Raul kwa sasa ndiye anayewatia makali chipukizi wa kikosi cha Real.

“Kuondoka kwa Zidane kutawapa Real jukwaa zuri la kuajiiri Allegri – kocha mzoefu aliye na uwezo wa kudhibiti presha na kudumisha nidhamu kambini,” ikasema sehemu ya taarifa ya gazeti hilo kwa kusisitiza kwamba Zidane atadumishwa tu na Real kambini mwao iwapo atawasaidia kutwaa taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Real wamepangiwa kuvaana na Atalanta ya Italia kwenye raundi ya 16-bora ya UEFA huku mchuano wa mkondo wa kwanza ukichezewa nchini Italia mnamo Februari 24.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kenya iliporwa Sh330.5 milioni ikipoteza pia uenyeji wa...

Lampard, Terry na Vieira wapigania nafasi ya kuwa kocha wa...