• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
Leicester kutegemea zaidi Maddison na Perez dhidi ya Southampton

Leicester kutegemea zaidi Maddison na Perez dhidi ya Southampton

Na MASHIRIKA

KOCHA Brendan Rodgers amesema wanasoka James Maddison, Hamza Choudhury na Ayoze Perez wana fursa ya kujifuta tope uwanjani na kujirejeshea sifa baada ya kukiuka kanuni za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Watatu hao walikuwa sehemu ya wachezaji waliotemwa na Leicester kwenye kikosi kilichopoteza mchuano uliopita wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) dhidi ya West Ham United.

Hata hivyo, masogora hao watakuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na Leicester kwenye nusu-fainali ya Kombe la FA dhidi ya Southampton mnamo Aprili 18 uwanjani Wembley, Uingereza.

“Lazima tusahau yaliyopita na kutazamia yajayo. Njia bora zaidi ya kufanya hivyo ni kujitakasa uwanjani kwa kujituma maradufu na kuletea kikosi mafanikio,” akasema Rodgers.

“Hawa ni baadhi ya wachezaji ambao wamekuwa tegemeo letu kwa kipindi kirefu. Tupo mahali tulipo kwenye msimamo wa jedwali kwa sababu ya upekee na ukubwa wa mchango wao,” akaendelea Rodgers.

“Walifanya kosa na katika soka, huwa kuna fursa ya kufanya maamuzi upya na ninaamini watajinyanyua na kuendelea kutambisha timu,” akaongeza.

Maddison amekuwa nguzo muhimu kambini mwa Leicester msimu huu baada ya kufungia kikosi hicho jumla ya mabao 11 na kuchangia 10 mengine katika mapambano yote.

Ufufuo wa makali yake ni kiini cha kocha Gareth Southgate wa timu ya taifa ya Uingereza kuwazia kuhusu uwezekano wa kutegemea maarifa yake kwenye fainali za Euro 2021.

Kwa upande wake, Perez amechangia mabao matatu kutokana na mechi 27 huku Choudhury akifunga goli moja kutokana na mechi 20 zilizopita.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Arsenal kukutana na Villarreal ya Unai Emery kwenye...

DOUGLAS MUTUA: Somalia ni mseto wa vituko na udikteta